Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SUA waja na mfumo mpya wa kuuza dawa za miti

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) upande wa taaluma, utafiti na ushauri wa kitaalamu Profesa Maulid Mwatawala akizungumza na wadau pamoja na watafiti wa mradi wa GRILI unaoshughulika na bidhaa zitokanazo na mimea.  Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Kutokana na kukua kwa biashara ya dawa za asili za miti zinazotumiwa nchini, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi wanatekeleza mradi wa kuongeza thamani bidhaa za mimea dawa, ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti

Morogoro. Kutokana na kukua kwa biashara ya dawa za asili za miti zinazotumiwa nchini, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi wanatekeleza mradi wa kuongeza thamani bidhaa za mimea dawa na mfumo wa mauzo ya dawa hizo.

 Hayo yameelezwa jana Februari 6 na Naibu Makamu anayeshughulika na taaluma, utafiti na ushauri, Profesa Maulid Mwatawala alipozungumza na Mwananchi baada ya kufunga mkutano wa wataalamu hao uliofanyika mkoani Njombe.

Amewapongeza watafiti wa mradi huo kwa kufanikiwa kufikia malengo matatu ambayo ni pamoja na kujengea uwezo watafiti, kuzalisha elimu mpya pamoja na kuzalisha mifumo mipya ya biashara kwenye eneo la mimea dawa.

Amesema katika mkutano huo wadau wote wa mradi kutoka ndani na nje ya nchi walikutana na kupokea matokeo ya mwisho ya mradi kutoka kwa wasimamizi wa mradi huo na wanafunzi waliokuwa wanasomeshwa na mradi wakifanya tafiti mbalimbali.

 “Tumefurahishwa na utekelezaji wa mradi huu ambao ulikuwa na malengo makuu matatu ya kujenga uwezo kwa watafiti wetu, kuzalisha  elimu mpya pamoja na mifumo mipya ya biashara kwenye eneo la mimea dawa ambayo ni muhimu kwa uchumi wa wadau kwenye mnyororo wa thamani wa mimea dawa nchini,” amesema Profesa Mwatawala.

Aidha, amesema kama chuo wamefarijika kuona mradi umezalisha wanafunzi watano wa shahada ya uzamivu kwenye masuala ya mimea dawa na saba wa shahada ya uzamili ambao kwa ujumla wameweza kuandaa machapisho ya kisayasi 17 kwenye eneo hilo muhimu.

Kufuatia mafanikio hayo Profesa Mwatawala amempongeza Mkuu wa mradi huo Profesa Faith Mabiki kwa kazi kubwa aliyoifanya na wasimamizi wengine wa mradi huo.

Amesema mfumo mzuri wa biashara ya bidhaa za mimea dawa uliotengenezwa na mradi huo utakuwa kichocheo kizuri cha mabadiliko na mafanikio ya biashara ya dawa asili, kwa kuwa zitaanza kuuzwa katika mifumo rasmi.

“Kitu kingine muhimu ambacho ni kizuri mradi huu umefanya ni kuwaunganisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa bidhaa za mimea dawa kupitia Jukwaa la Ubunifu wa Bidhaa zitokanazo na Mimea dawa (GRIP) ambalo limesaidia kuwaweka pamoja wadau wote na kujadiliana maendeleo na changamoto na kuzitatua kwa pamoja," amepongeza Profesa Mwatawala.

Kwa upande wake Mkuu wa Mradi huo, Profesa Faith Mabiki amesema mradi huo umejikita katika bidhaa zitokanazo na mimea dawa kwa maana ya tiba asili na mnyororo mzima wa thamani ili kusaidia Tanzania kunufaika na utajiri mkubwa ilionao wa maliasili hususani mimea dawa kwa kufikia soko la dunia.

Aidha amesema utafiti huo ulilenga kusaidia Tanzania kufikia mpango wake wa maendeleo endelevu wa 2025 unaotambua mchango wa matumizi ya maliasili ikiweo mimea dawa ambayo ipo nchini na inatumiwa lakini haijaweza kushika vyema soko la ndani na kimataifa na kuchangia maendeleo ya wadau wa tiba asili.

Hata hivyo ametaja changamoto kubwa iliyoletwa na utafiti unaofanywa na mradi huo ni namna ambavyo sasa wanaweza wakachukua matokeo ya mradi huo ili kuyakuza kuleta maendeleo ya wadau binafsi katika kuongeza ubora na masoko.

Profesa Mabiki ameeleza wanajivunia na kufanikiwa kupata kifaa cha kisasa cha kupima kemikali za mimea dawa, madawa na vyakula ambacho kitaendelea kusaidia watafiti, wanafunzi na wadau wengine kukikutumia katika kufanya tafiti mbalimbali hapahapa nchini.