Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Elon Musk atoa angalizo kuhusu AI

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Asema mifumo ya AI inaweza kufikia uwezo mkubwa wa kufanya kazi za kiakili ambazo kwa sasa zinafanywa na binadamu, ikiwamo utafiti wa kisayansi, uandishi, uhandisi, upangaji mikakati na programu za kompyuta.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara na mwekezaji wa teknolojia, Elon Musk amesema Akili Unde (AI) inaweza kufikia kiwango cha kuzidi uwezo wa akili ya pamoja ya binadamu ndani ya miaka mitano ijayo.

Amesema hali itaifanya dunia kuingia katika hatua mpya ya mapinduzi ya teknolojia ndani ya miaka michache ijayo.

Kauli hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu kasi ya maendeleo ya teknolojia hiyo, huku wataalamu wakitafakari namna ya kuhakikisha AI inaendelea kutumika kwa manufaa ya binadamu bila kuleta madhara kwa jamii.

Musk, ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya magari ya umeme ya Tesla na kampuni ya teknolojia ya akili unde ya xAI, amesema maendeleo ya AI yanaenda kwa kasi kubwa kuliko ambavyo watu wengi wanavyoweza kufikiria.

Katika mahojiano yake na jarida la The Economist, Musk amesema mifumo ya AI inaweza kufikia uwezo mkubwa wa kufanya kazi za kiakili ambazo kwa sasa zinafanywa na binadamu, ikiwamo utafiti wa kisayansi, uandishi, uhandisi, upangaji mikakati na programu za kompyuta.

Amesema kutokana na kasi hiyo, kuna umuhimu kwa kampuni kubwa zinazotengeneza teknolojia hiyo kushirikiana katika kuhakikisha usalama wake unazingatiwa kabla ya mifumo mipya kuachiwa kwa matumizi ya umma.

Musk amependekeza kampuni hizo ziwe na utaratibu wa kukagua mifumo kabla ya kuitoa sokoni, hatua anayodai inaweza kusaidia kubaini changamoto za kiusalama mapema.

Amesema kampuni hizo zinapaswa kufanya majadiliano ya mara kwa mara kuhusu usalama wa AI, kubadilishana taarifa kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza na kuruhusu tathmini za kitaalamu baina yao.

“Watengenezaji wa teknolojia hii wana uelewa mkubwa wa kutambua uwezo na hatari zinazoweza kujitokeza kuliko kusubiri serikali kuingilia kila hatua ya maendeleo ya AI, hivyo ni vyema kukawa na utaratibu wa kukagua mifumo kabla ya kuitoa,”amesema Musk.

Hata hivyo, suala la usalama wa AI limeendelea kuwa mjadala mkubwa duniani, huku baadhi ya wataalamu wakihofia kuwa mifumo yenye uwezo mkubwa inaweza kutumika vibaya endapo hakutakuwa na kanuni na mifumo madhubuti ya udhibiti.

Fursa na hofu ya AI

Wakati baadhi ya watu wakiona AI kama tishio kwa ajira na nafasi ya binadamu katika soko la kazi, wengine wanaamini teknolojia hiyo inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo katika sekta mbalimbali.

Musk amesema AI inaweza kuleta kipindi cha ongezeko kubwa la uzalishaji na ustawi wa kiuchumi, ambapo mashine zitaweza kusaidia kufanya kazi nyingi kwa ufanisi mkubwa.

Teknolojia hiyo tayari imeanza kubadilisha namna watu wanavyofanya kazi katika maeneo kama elimu, afya, biashara, uandishi, utafiti na huduma za kifedha.

Katika elimu kwa mfano, AI imesaidia wanafunzi kupata msaada wa kujifunza, kutengeneza maudhui na kufanya tafiti kwa haraka.

Hata hivyo, imeibua pia changamoto kuhusu matumizi yasiyo sahihi kama udanganyifu wa mitihani na utegemezi wa mashine badala ya kujenga uwezo wa kufikiri.

Kwa nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, wataalamu wa teknolojia wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kujiandaa mapema kwa kuwekeza katika ujuzi wa kidijitali ili wananchi waweze kutumia fursa zinazotokana na AI.

Hivi karibuni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema matumizi ya Akili Unde yataendelea kuhamasishwa katika kujifunza na kufundishia, lakini yatumike kwa kuzingatia maadili na si kama njia ya kufanya udanganyifu.

"Fikiria unaenda kutibiwa na daktari aliyefaulu kwa kudanganya kwenye mitihani. Hilo ndilo tunalopambana nalo ili kuhakikisha wahitimu wetu wana ujuzi wa kweli," amesema Profesa Mkenda.

Mtaalamu wa teknolojia Deus Ngaruko amesema mjadala kuhusu AI unahitaji kuangalia namna ya kuhakikisha teknolojia hiyo haiongezi pengo kati ya wanaomudu teknolojia na wale wasio na uwezo wa kuipata.

“Teknolojia mpya mara nyingi huanza kunufaisha wale wenye rasilimali zaidi. Watu wenye kompyuta, intaneti ya uhakika na uwezo wa kulipia huduma za AI wana nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji, kujifunza ujuzi mpya na kupata ajira zenye kipato kikubwa.

“Kwa upande mwingine wasioweza kumudu vifaa hivyo wanaweza kubaki wakitumia mbinu za zamani, jambo linaloongeza tofauti ya kipato kati ya makundi hayo,” amesema Ngaruko.