SUA, washirika wa maendeleo nchi 15 wafanya tafiti kuangazia sera za kibiashara, matokeo ya uchumi
Morogoro. Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kutoka nchi 15 za Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kusini wamefanya utafiti na kubainisha faida na hasara za kiuchumi, kimazingira na kijamii zinazotokana na utekelezaji wa sera za kibiashara na matokeo ya uchumi.
Utafiti huo uliofanywa na SUA kupita ndaki ya uchumi na stadi za biashara, unaofadhiliwa na mfuko wa utafiti wa changamoto duniani (The global challenges research Fund-GCRF) na mfuko wa pamoja wa utafiti na ubunifu wa Uingereza (UK Research and Innovation –UKRI- collective fund) umeangazia masuala ya biashara, maendeleo na mazingira ukigusia pamoja na mambo mengine mazao ya kahawa, soya, sukari na wanyamapori.
Mkuu wa mradi wa Biashara, Maendeleo na Mazingira (Trade, Development and Environment- TRADE Hub Project) Profesa Reuben Kadigi amebainisha hayo mjini Morogoro wakati akiwasilisha taarifa ya utafiti huo.
Profesa Kadigi amesema kuwa mradi huo umelenga kufungamanisha shughuli za biashara na bidhaa za kilimo na wanyamapori ili biashara zinazofanyika ziwe kichocheo cha ukuaji shirikishi wa uchumi na kupunguza umaskini kufikia maendeleo endelevu bila kusababisha ongezeko la uharibifu wa mazingira na wa bayoanuwai zilizopo.
Amesema nia ni kuwezesha nchi kuwa na sera na mikakati endelevu iliyofanyiwa utafiti.
Profesa Kadigi amesema mradi huo wa miaka mitano, ulianza kutekelezwa Februari 2019 hadi Machi 2024 ambapo matokeo ya utafiti huo yanalenga kutaarifu na kuwezesha kupatikana kwa sera na mikakati endelevu ya biashara ya bidhaa zilizofanyiwa utafiti.
Akimwakilisha mkuu wa Ndaki ya Uchumi na stadi za biashara ya chuo kikuu cha Sokoine, Naibu Mkuu wa ndaki hiyo, Dk Zena Mpenda amesema,uchaguzi wa bidhaa zilizofanyiwa utafiti za kilimo na wanyamapori, ulizingatia umuhimu wa changamoto za kibiashara unaozikabili tasnia hizo ambapo wadau wataangalia matokeo ya tafiti hizo na kutoa mapendekezo ya namna ya kuzitatua.
Akatolea mfano wa zao la kahawa kama miongoni mwa mazao makuu ya jadi ya kibiashara, limepitia changamoto nyingi sana kimasoko zilizosababisha kushuka kwa tija na kipato kwa wazalishaji na wauzaji,ambapo takwimu za mkutano wa umoja wa mataifa wa biashara na maendeleo mwaka 2018, zinaonesha kuwa kati ya miaka 1980 hadi 1995,wakulima wa kahawa walidhibiti takribani asilimia 20 ya mapato yote katika mnyororo wa thamani wa zao hilo na asilimia 55 zilibaki kwa wanunuzi.
“Lakini mwaka 1989,soko la kahawa la kimataifa lilirekodi kushuka kwa kasi kwa bei ya kahawa ya kimataifa kwa asilimia 49 na kuchangia kukosekana kwa usawa katika kugawana ongezeko la thamani katika mnyororo wa thamani wa kahawa duniani kwa gharama za nchi zinazozalisha zao hilo,na uzalishaji kwa bara la Afrika ukashuka kwa asilimia 35 hivyo wakulima wengi wadogo wakahamia kwenye mazao mengine salama na yenye faida, wengine walikata miti ya kahawa na kupanda mazao mbadala” amesema Dk Mpenda
Kuhusu sukari amesema imekuwa na changamoto za mbalimbali za kubadilika kwa bei kutokana na udhibiti wa nchi chache za Brazili na Thailand zinazouza zaidi ya nusu ya sukari yote kwenye soko la dunia, huku nchi nyingi ikiwemo Tanzania, zikikumbwa na mabadiliko ya tabia nchi hasa upungufu wa mvua unaoathiri pia uzalishaji wa miwa.
“Haya mabadiliko yamekuwa yakituathiri moja kwa moja kwasababu bado tunahitaji kuingiza kiasi kikubwa, na hali hii imesababisha tupokee mabadiliko kadhaa katika utekelezaji wa sera za biashara," amesema
Amesema "hivi karibuni kulikuwa na changamoto ya sukari ya viwandani kutokana na upungufu wa makasha ama kontena katika baadhi ya nchi wazalishaji, mahitaji ya sukari Tanzania na duniani pia yamekuwa yakiongezeka,duniani yamefikia tani 185 milioni, hii ni fursa kubwa ndio maana Serikali ina mikakati madhubuti kuongeza uzalishaji ili kufikia utoshelevu na kuuza nje,” ameongeza.
Akasema jitihada nyingine zinazoendelea kufanywa ziko pia kwenye mazao mengine ikiwemo Soya ambapo mwaka 2020 Novemba, Serikali iliingia makubaliano ya kuuza soya nchini China ingawa uzalishaji wa zao hilo bado una changamoto ikiwemo uzalishaji mdogo wa tani 44,106 kwa mwaka 2021, tija ndogo kwa uzalishaji wa kiwango cha 0.66 za tani kwa hekta, maeneo madogo ya wazalishaji kwa wastani wa hekta 0.96 kwa kila mzalishaji, huku gharama za uzalishaji za dola 319 kwa tani moja.
Dk Mpenda amesema imewafanya wakulima wa soya kushindwa kushindana katika kuchangamkia soko la ndani ambalo mahitaji yake kwa sasa ni tani 150,000 kwaajili ya chakula cha mifugo na masoko ya nje.
Baadhi ya watafitim akiwemo Mtafiti Mkuu, Profesa Japhet Kashaigili na amesema kinachofanyika sasa ni kukusanywa kwa takwimu na kutoa mapendekezo juu ya nini kifanyike baada ya matokeo ya utafiti ili kusaidia kupatikana kwa sera bora zitakazojali mazingira na wanyamapori.
Profesa Kashaigili amesema wanachohitaji sasa ni kuwa na mpango ama utaratibu wa kufikia mahitaji halisi na wameweka mafanikio sita muhimu waliyobaini yatasaidia kuwa na sera na mazingira bora katika tasnia hizo.