Polisi yakamata 130 kwa tuhuma za ugaidi, 36 kortini
Muktasari:
- Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema watuhumiwa 36 wamefikishwa mahakamani, wakiwemo watu wanne waliokamatwa mkoani Iringa wakiwa na vilipuzi 155, huku watuhumiwa wengine wakiendelea kufikishwa mahakamani.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema limewakamata watu 130 katika mikoa mbalimbali kwa tuhuma za kupanga na kuhamasisha vitendo vya kihalifu vinavyohusishwa na ugaidi.
Vitendo hivyo ni kupanga kufanya fujo kupitia maandamano yasiyofuata sheria, kuua viongozi wa Serikali, kuchoma shule, kulipua miundombinu ya umeme na kushambulia askari ili kupora silaha.
Pia, jeshi hilo limesema linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliotajwa katika ushahidi uliokusanywa.
Hayo yameelezwa kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo, Jumapili, Julai 26, 2026, na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.
Misime amesema watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na ufuatiliaji uliofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama katika majukwaa mbalimbali, yakiwemo mitandao ya kijamii, waliobainika wakipanga na kuhamasisha vitendo vya uhalifu.
"Ushahidi uliokusanywa kupitia njia mbalimbali unaonesha kuwapo kwa njama zilizokuwa zikipangwa kupitia mikutano ya ana kwa ana, mijadala ya klabu za mitandaoni, pamoja na kusambaza jumbe na vipeperushi vinavyohamasisha vitendo vya vurugu na uhalifu," amesema Misime.
Amesema uchunguzi umebaini kuwa, mbali na kupanga kufanya fujo kupitia maandamano yasiyofuata sheria, watuhumiwa hao walidaiwa kupanga kuua viongozi wa Serikali na wananchi wasiowaunga mkono.
Pia, walidaiwa kupanga kuchoma shule ili kuleta hofu kwa wazazi na walezi, kulipua transfoma za umeme, kukata miti ili kuziba barabara na kuharibu mali za umma na za binafsi.
Misime amesema watuhumiwa hao pia wanadaiwa kupanga kushambulia askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha na kuzitumia kutekeleza malengo yao, hali ambayo, kwa mujibu wa ushahidi uliopo, inabeba viashiria vya makosa ya kigaidi.
Amesema kwa mujibu wa sheria, vitendo vya kigaidi vinajumuisha kula njama, kupanga na kuhamasisha vitendo vinavyolenga kueneza hofu kwa wananchi, kujeruhi au kuua watu, kupora silaha na kuharibu miundombinu muhimu ya nchi.
Washtakiwa 23 wanaoshtakiwa katika kesi mbili tofauti zenye kosa moja la kujihusisha na mikutano au mazungumzo yanayoweza kupelekea ugaidi walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza. Picha na PraiseGod Mgumba
Kwa mujibu wa Misime, hadi sasa watuhumiwa 36 wamefikishwa mahakamani, wakiwemo watu wanne waliokamatwa mkoani Iringa wakiwa na vilipuzi 155, huku watuhumiwa wengine wakiendelea kufikishwa mahakamani, na baadhi wakiendelea kusakwa kutokana na ushahidi uliokusanywa.
"Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuhakikisha Watanzania na Taifa letu vinaendelea kuwa salama," amesema Misime.
Licha ya taarifa ya Polisi kutowataja hao 36 waliopandishwa kizimbani kwa ugaidi, miongoni mwa washtakiwa hao wamo wanafunzi wanne wa vyuo vikuu tofauti mkoani Mbeya, wengine jijini Mwanza, pamoja na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Wanafunzi hao walioshtakiwa kwa kosa hilo lisilo na dhamana ni Noah Mwalwange (23), mkazi wa Isange na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Gwamaka Mboka (28), Rojazi Mpwani (21) na Augustino Wasinyo (25), wote wa Chuo Kikuu cha Katoliki (CUoM).
Wanafunzi hao kwa pamoja walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Paul Rupia wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Julai 23, 2026, na kusomewa shtaka la kushiriki katika vitendo vya kigaidi.
Baadhi ya washtakiwa hao ni viongozi wa Chadema, na kesi zao zilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Naibu Msajili Erick Marley.
Katika kesi ya kwanza namba 16379/2026, washtakiwa 13 kutoka Wilaya ya Ilemela wanashtakiwa kwa kufanya kosa hilo kati ya Juni 25 na Julai 7, 2026.
Kwa mujibu wa Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadi, kati ya watuhumiwa hao 23, wanane ni viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho kuanzia kata hadi matawi katika wilaya za Nyamagana na Ilemela.
Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Gaston Garubindi, alisema hadi Ijumaa, Julai 24, 2026, makada na viongozi 27 wa mikoa ya Mwanza na Mbeya walikuwa wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi.
Pia, Julai 23, 2026, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedek Kaijage, alifikishwa mahakamani jijini Dodoma akishtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi na ugaidi.
Mhadhiri huyo alifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule, na kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 5, 2026, itakapotajwa.