Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sukari bado kivumbi, watu wanunua kwa foleni

Dar/Mikoani. Bei ya sukari ni mfupa ulioishinda Serikali? Hili ndilo swali linaloumiza vichwa vya watu nchini, baada ya kuendelea kupaa na kufikia hadi Sh6,000 kwa kilo katika baadhi ya mikoa, licha ya kutangazwa bei elekezi nchini.

Jijini Mwanza leo Februari 14 wafanyabiashara wamepanga foleni kwa zaidi ya saa 10 kununua sukari, huku baadhi ya mikoa ikishuhudiwa kilo moja ya sukari ikiuzwa hadi Sh6,000 badala ya bei kikomo ya Sh3,200.

Januari mwaka huu, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliutangazia umma kuwa, Serikali ilikuwa imeruhusu kuingizwa nchini tani 50,000 za sukari Januari na Februari 2024,  kama njia ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa sukari.

Kupitia taarifa yake hiyo, Waziri Bashe alisema uzalishaji wa sukari nchini umeshuka kuanzia Novemba 2023 kutokana na mvua nyingi zilizonyesha na kusababisha kushindwa kuvunwa miwa na viwanda kusitisha uzalishaji.

Januari 23, 2024, Serikali kupitia kwa mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Keneth Bengesi ilitangaza bei elekezi kuanzia Sh2,700 kwa kilo na haikutakiwa kuzidi Sh3,200 kwa kilo kwa rejareja, hata hivyo kiwango hicho hadi sasa hakijafikiwa.


Leo kwa foleni

Wafanyabiashara wa sukari jijini Mwanza wamepanga foleni kwa zaidi ya saa 10 ili kununua bidhaa hiyo kwa Kampuni ya V. H. Shah & Co ambayo ndiyo msambazaji mkuu wa bidhaa hiyo kanda ya ziwa.

Bei ya sukari mkoani Mwanza ni kati ya Sh4,000 hadi 5,000 kwa baadhi ya maeneo.

Wakiwa wamepanga foleni, wamesema wamefika kwenye kampuni hiyo tangu saa 11 alfajiri, lakini mpaka saa tisa alasiri walipozungumza na gazeti hili walikuwa hawajapata sukari kutokana na idadi kubwa ya waliokuwa kwenye foleni.

"Nimekuja hapa tangu asubuhi, lakini mpaka sasa sijapata sukari. Huko mtaani bei mfuko mkubwa wa kilo 50 wanauza Sh220,000 na hapa wanauza Sh164,000,  sasa fikiria huyu mfanyabiashara akinunua anaenda kuuzaje huko mtaani? Akiuza Sh6,000 wanamuita mhujumu uchumi na anakamatwa, sasa Serikali haioni wanaoleta sukari wanauzaje, lakini inawaona tu wanaopandisha ili angalau fedha zao zirudi,” amesema Juma Shaban, mfanyabiashara mdogo kutoka Machinjioni, jijini Mwanza.

Ofisa Biashara Mkoa wa Mwanza, Yessaya Sikinde alipotafutwa kuzungumzia sakata la sukari jijini Mwanza, amedai yupo kwenye kikao kujadili suala la sukari, kikao ambacho kitatoa maazimio nini kifanyike, akiahidi kutoa mrejesho baada ya kikao hicho.

"Saa hii tunavyoongea na wewe tupo kwenye kikao hicho hicho, nafikiri tutakuwa na maazimio, kwa sasa nisiseme, tusubiri nini kikao kitaamua na nitakutafuta," amesema Sikinde, alipotafutwa tena hakupatikana.

Jiji la Dar es Salaam katika Wilaya ya Ilala imefikia Sh5, 400 kwenye baadhi ya maduka.

Mfanyabiashara wa Kimara, Sairis Sebastian amesema bidhaa hiyo haipatikani.

Mkoani Kilimanjaro sukari inauzwa kati ya Sh5,000 hadi Sh5,500 katika baadhi ya maeneo.

Neema Kavishe, mkazi wa mkoa huo amedai sukari imefika mahali imekuwa kama lulu kutokana na gharama yake kuwa kubwa na wanapowauliza wamiliki wa maduka kwa nini wanauza ghali wanajibiwa kuwa ni kutokana na bei wanayonunulia sokoni. Sehemu nyingi inauzwa hadi Sh6,000 kwa kilo.