Wafanyabiashara ‘wagombania’ sukari Mtwara

Muktasari:

  • Wafanyabiashara Mtwara wagombania sukari iliyopelekwa na Serikali kwa lengo la kupunguza uhaba wa upatikanaji wa bidhaa hiyo, wasema kiwango walichopelekewa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji

Dar es Salaam. Wafanyabiashara mkoani Mtwara wamegombania  sukari iliyopelekwa na Serikali kwa lengo la kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo

Serikali imepeleka tani 52 za sukari kupitia wafanyabiashara na walikuwa wanauza mfuko mmoja wa kilo 50 kwa Sh140,000 hadi Sh150,000, kwa kuzingatia maelezo ya Serikali ili kupunguza kero ya upatikanaji wake.

Kwa maana hiyo, wafanyabiashara watakwenda kuuza kilo moja ya sukari kwa Sh2,800 hadi Sh3,000 kama ambavyo Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) ilivyotoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali juu ya bei elekezi kwa rejareja na jumla.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na  kituo cha runinga cha Azam jana usiku Jumanne, Februari 13, 2024 imesema Mtwara kuna uhaba wa sukari  na kwa baadhi ya maeneo inakopatikana kilo moja inauzwa hadi Sh6,000.

Mfanyabiashara Said Tandi amesema kugombania kwao kumesababishwa na kuwepo kwa foleni kubwa ya wafanyabiashara wanaohitaji bidhaa hiyo, huku kila mmoja akitaka kupata nyingi.

“Sukari iliyofika ni kidogo ilihali  mahitaji ni makubwa na mazingira tunayotoka hali ni mbaya zaidi, ndiyo maana kuna kugombania kila mmoja anataka apate,” amesema Tandi

Mfanyabiashara mwingine Ally Madidima amesema wanashukuru Serikali kwa kuwapelekea sukari, lakini ombi lao bado uhitaji wa bidhaa hiyo Mtwara ni mkubwa.

“Kama kuna namna wanaweza kufanya basi Serikali iongeze  sukari nyingine kwani wananchi wanataabika kutafuta lakini haipatikani,” amesema.

Naye Ibrahimu Alfani ambaye ni mfanyabiashara amesema kiwango cha tani walichokipata bado hakitoshi kwani mkoa huo ni mkubwa na una watu wengi.

“Kwa sukari niliyopata yote imeshaisha na ukiangalia bado wateja ni wengi dukani kwangu sijui nitawaambia nini maana hata hawaelewi,” amesema.

Amesema katika kugombania huko alifanikiwa kupata mifuko 530 na yote ameshaiuza na bado wateja wanahitaji.