Sumaye azindua wiki ya Hanang' kwa kuwaonya wanasiasa
Muktasari:
- Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye amezindua maadhimisho ya wiki ya maendeleo Hanang' kwa kuwataka wanasiasa kuacha kutumia kipindi cha uchaguzi kuingilia na kuharibu mshikamano uliopo kati ya wananchi na Serikali.
Hanang'. Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye amezindua maadhimisho ya wiki ya maendeleo Hanang' kwa kuwataka wanasiasa kuacha kutumia kipindi cha uchaguzi kuingilia na kuharibu mshikamano uliopo kati ya wananchi na Serikali.
Sumaye amesema baadhi ya wanasiasa husababisha hali hiyo na kukwamisha maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujitoa kwa michango mbalimbali inayoanzishwa na Serikali.
Sumaye ameyasema hayo akizindua maadhimisho ya wiki ya maendeleo wilayani Hanang' mkoani Manyara.
Maadhimisho hayo yamehusisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kupata michango ya uboreshaji hospitali ya Wilaya ya Hanang' iitwayo Tumaini.
Amesema kipindi cha uchaguzi wanasiasa wamekuwa wakiingilia na kukwamisha mipango mbalimbali ya Serikali na kurudisha nyuma muamko wa wananchi kujitoa kuchangia maendeleo yao.
"Muda mchache kabla ya kufika uchaguzi kila diwani hutaka jambo ambalo haliwezekani lifanyike na kuona watumishi wa Serikali hasa mkurugenzi anawarudisha nyuma na kuzua mizozo," amesema Sumaye.
Hata hivyo, amepongeza juhudi za ubunifu uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang', Janeth Mayanja katika kuiweka wilaya hiyo mikono salama .
Mkuu wa wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja amewashukuru wadau wote wa maendeleo walioshiriki na kujitolea vifaa vya ujenzi ambapo mifujo ya saruji 1,120 imepatikana.