Prime
Taarifa tsunami ilivyozua taharuki Dar
Dar es Salaam. Asante Mwenyezi Mugu. Ni maneno ambayo pengine wakazi wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam, waliyatamka juzi baada ya kutotokea kwa janga la tsunami.
Taarifa iliyosambaa juzi mitandaoni ikitahadharisha kuwapo kwa tukio la tsunami, ilizua hofu na taharuki miongoni mwa wakazi wa mwambao wa Pwani, wakati Serikali ikisema haikuwa taarifa rasmi kwa umma.
Mbali na taarifa hiyo iliyoonyesha kuandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilikuwepo pia video iliyomuonyesha mmoja wa maofisa akiwa amekaa na watu wanaoonekana kuwa ni askari wa Jeshi la Polisi akifanya mawasiliano kuhusu tishio la tsunami, hivyo kuzidi kuleta hofu zaidi.
“Tumepata taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, kiwango cha kutokea tsunami ni uhakika kwa upande wa maeneo ya Msasani, Wilaya ya Kinondoni pamoja na Wasukutani, Wilaya ya Kigamboni yanategemewa kuathirika zaidi... wananchi wa eneo hilo waondoke haraka,” alisikika akisema ofisa huyo.
Pia aliagiza vyombo vya taasisi mbalimbali za uokozi na kupambana na maafa ziwe katika hali ya juu ya kasi ya utayari.
Kufuatia taarifa hiyo, wakazi wa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, hasa Msasani, Kunduchi, Bunju, Mbweni, Ununio, Kigamboni, Mikocheni na kwingineko walikumbwa na hofu na taharuki.
Simulizi za wakazi
Akisimulia mkasa huo, Edwin Mtalemwa, mkazi wa Pugu alisema; “Baba mkwe wangu alikuwa na ratiba ya kulala Kunduchi kwa dada yake, akawa ameshafika huko lakini akapata ile taarifa kupitia mitandao ya kijamii. Nyumba ya dada yake ipo karibu sana na bahari, aliamua kuondoka huko kurudi Pugu na alifika nyumbani saa 5 usiku.”
Joseph Moshi, mkazi wa Masaki alisema baada ya kusoma taarifa ile mtandaoni, alishtuka lakini kwa kujiridhisha zaidi, aliamua kutafuta zaidi mtandaoni, hasa habari za kimataifa kujiridhisha kama kweli kuna tetemeko baharini linaloweza kuleta tsunami upande wa Tanzania.
“Sikuona, ila bado nilijawa na wasiwasi kwa sababu niliwaza kama inapiga, basi wakazi wa Masaki ni waathirika wa kwanza,” alisema Moshi.
Naye Asia Mohamed akizungumzia hilo, alisema taarifa hiyo aliipata akiwa nje ya nyumbani kwake. “Niliwaza nafikaje kwa haraka nyumbani Mbweni nikawachukue wanangu niwapeleke Kibaha kwa mdogo wangu tusubirie huko.”
Asilimia kubwa ya waliozungumza na Mwananchi walisema taarifa ile ilizua taharuki kubwa.
Meneja Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA Dk Mafuru Kantamla, alisema walipokea simu nyingi kutoka kwa wananchi na waandishi wa habari waliotaka ufafanuzi wa taarifa hiyo.
Lakini juzi usiku, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenister Mhagama aliwataka wananchi kupuuza taarifa hiyo, akisema haikuwa rasmi kwa umma.
Aliyasema hayo alipozungumza na Kituo cha televisheni cha Azam. Alisema wataalamu wa masuala ya hali ya hewa wanaendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na mvua za El Nino.
“Taarifa kuhusu tsunami sio rasmi na Ofisi ya Waziri Mkuu, imewasiliana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuthibitisha hakuna tsunami na wala hakuna utabiri wowote kuhusu Tsunami,” alisema Waziri Jenister.
Wataalamu wa majanga
Hata hivyo, wataalamu wa majanga wanasema licha ya kuwa taarifa hiyo haikuwa ya kweli, bado kuna haja kwa Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2022 kuanza kutekelezwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayokuja na majanga anuai.
Mtaalamu wa majanga, James Mbatia anasema: “Kwa hali ilivyo sasa, kuna haja kwa kila Mtanzania kujua kuhusu majanga, athari zake na namna ya kujikinga nayo, siyo kusubiri mpaka yatokee, watu wapatiwe elimu rasmi na isiyo rasmi kupitia vyombo vya habari.
Aliongeza: “Sheria hii ifanye kazi, tunatakiwa tuwe na asasi kama ilivyo mamlaka nyingine. Sheria ipo lakini Serikali haijataka kuisimamia.’’
Alisema majanga kama tsunami yanapotokea, kuna namna ya kujikinga, taarifa kwa umma ni jambo moja, lakini kuukinga umma ni jambo jingine.
Aliongeza kuwa nchi yetu imeweka nguvu kubwa katika kupambana na majanga kuliko kukinga.
“Tsunami ikipiga ufukwe wa bahari ya Hindi pwani yetu ina urefu wa kilomita 1,424 kutoka Mtwara mpaka Tanga, kwa urefu huo unaweza kuona athari kwetu ilivyo kubwa,” alisema.
Mtaalamu mwingine wa majanga, Dk Amos Mteganzi alisema ni vizuri Serikali ikaonyesha namna inavyojitayarisha na majanga kama hayo, huku akionyesha wasiwasi wa uhalisia huo.
“Kumekuwepo na mfululizo wa majanga miaka ya hivi karibuni, ambayo yameacha maswali mengi kwenye jamii kuhusu utayari na uwezo wa nchi yetu kupambana nayo kwa kuokoa watu au kupunguza athari, hiki walichokifanya nakiona kama sio cha muhimu kwa sasa.
“Tunahitaji wajifungie kimyakimya wafanye utayari na tafiti zao kisha watoke na majawabu,” alisema Dk Mteganzi.
Tsunami ni nini?
Tsunami ni wimbi kubwa katika bahari linalosababishwa na tetemeko la ardhi, mlipuko wa volkano au matokeo mengine yanayoleta mshtuko wa ghafla chini ya maji. Mshtuko huo unasababisha kutokea kwa wimbi kali linaloanza kupaa juu likifika katika maji kame na kwenye ufuko wa bahari.
Miaka 10 imepita tangu bara la Asia likumbwe na kimbunga chenye upepo mkali kilichojulikana kama Tsunami. Upepo huo ulikua unakwenda kwa kasi kati ya kilomita 500 na 800 kwa saa na takribani watu 226,000 walifariki katika eneo la Asia ya Kusini.