Taasisi, mashirika ya umma yaongeze mchango serikalini

Thursday December 24 2020
masokopic
By Mwandishi Wetu

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametoa siku tisa kwa wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kujieleza kwa nini wamechangia kidogo kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

Dk Mpango amesema utekelezaji wa agizo hilo unaanza Desemba 22 na mwisho ni Desemba 30 kwa wakuu hao kueleza sababu za kutozingatia ukomo wa asilimia 60 kwenye matumizi yao yatokanayo na mapato ghafi kwa mujibu wa sheria.

Waziri amesema hayo alipokutana na wakuu wa taasisi za Serikali na mashirika 236 ya umma katika mwendelezo wa mikutano yake ya kikazi kutoa mwelekeo mpya wa utendaji utakaoimarisha na kuongeza mapato ya Serikali.

“Michango wa taasisi na mashirika ya umma kwenye mfuko mkuu wa Serikali bado hauridhishi. Mwaka 2019/20, mchango wenu ulikuwa chini ya asilimia moja, kiwango kidogo kikilinganishwa na uwekezaji uliofanywa na Serikali,” amesema Waziri Mpango.

Katika kusimamia hilo, amemwagiza msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka kuhakikisha taarifa ya wakuu hao inamfikia Desemba 31. Vilevile alitangaza kufuta likizo za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa viongozi hao ili watekeleze maelekezo aliyoyatoa.

Sheria ya Fedha ya mwaka 2015 na Sheria ya Msajili wa Hazina iliyorekebishwa mwaka 2015, zinaweka ukomo wa gharama za uendeshaji wa taasisi na mashirika ya umma yasiyo ya kibiashara kutozidi asilimia 60 ya mapato ya ghafi lakini zipo zinazovunja sheria hizo.

Advertisement

“Punguzeni matumizi yasiyo ya lazima ikiwemo misafara ya watendaji na wajumbe wa bodi kutembelea miradi ili kuziwezesha taasisi zao kuwa na fedha za kuchangia kwenye mfuko mkuu wa Serikali kugharamia miradi inayotekelezwa nchini,” amesema.

Aidha, waziri ampongeza msajili wa Hazina kwa kusimamia urejeshaji wa mali za Serikali zilizokuwa zinamilikiwa na watu binafsi bila kufuata sheria.

“Hadi Juni 30, mali zisizohamishika 1,562 zilikuwa zinashikiliwa au kumilikiwa kinyume cha sheria. Mali hizo zipo kwenye mikoa 19 iliyohakikiwa na zinajumuisha nyumba 862, viwanja 559, mashamba 43, kampuni mbili na maghala 96.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwaidi Alis Khamis aliwataka watendaji hao kuepusha ukiukaji wa maadili na matumizi mabaya ya fedha za Serikali na kuonya kuwa havivumiliki.

“Serikali ina matarajio makubwa kwenu. Wananchi masikini wanaondokana na hali hiyo kwa kuboresha maisha yao na kwamba mambo hayo yatawezekana kutokana na utendaji wao mzuri ikiwamo kukusanya ipasavyo mapato ya Serikali.

Kwa upande wake, Mbuttuka amemhakikishia waziri kwamba maelekezo aliyoyatoa yatafanyiwa kazi.


Advertisement