Taasisi ya Ruge Mutahaba kuzindulia Juni 26

Thursday June 23 2022
rugeepiic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Miaka mitatu baada ya kifo cha aliyekuwa mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba, taasisi iliyobeba jina lake inatarajiwa kuzinduliwa Juni 26 mwaka huu ikilenga kuendeleza kazi alizokuwa akifanya katika kuwasaidia vijana na jamii kwa ujumla.

Pamoja na kuwashika mkono vijana wabunifu taasisi hiyo inakuja kuendeleza maono aliyokuwa nayo Ruge katika kukuza ustawi wa wanawake na jamii kwa ujumla.

Mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Ruge Mutahaba Foundation, Georgia Mutaghaywa amesema lengo kubwa la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuendeleza vipaji vya vijana kama ambavyo alikuwa akipenda kufanya Ruge.

“Tunachoenda kufanya ni kukuza na kuendeleza vipaji na tutashirikiana na sekta binafsi, serikali na wadau  katika kuwaunganisha na fursa mbalimbali  vijana hawa waliojaliwa vipaji na ubunifu tukiendeleza maono ya Ruge, tunaomba watanzania waichukulie taasisi hii kama yao,”amesema Georgia.

Akizungumzia ujio wa taasisi hiyo kwa niaba ya familia ya Ruge, Rwebu Mutahaba amesema ndugu yao alijitahidi kuwekeza katika ubunifu na ujasiriamali wa vijana hivyo kuna kila sababu ya kuendeleza maono hayo.

“Tunachoomba kama familia jamii muipokee taasisi hii pamoja na kumuenzi ndugu yetu inakwenda kuendeleza yale mazuri yote ambayo alianzisha kubwa zaidi ikiwa kuwasaidia vijana,”amesema Rwebu.

Advertisement

Kwa upande wake  Suma Mwaitenda ambaye ni mkurugenzi wa Fursa kampeni iliyoanzishwa  na Ruge, amesema mojawapo ya changamoto zinazowasumbua vijana na wanawake ni ukosefu wa ajira hivyo taasisi hiyo imetengeneza mkakati wa kuendesha miradi utakaoyasaidia makundi hayo.

Kando na hilo amesema taasisi hiyo itatoa ufadhili wa masomo na ushauri wa kitaaluma kwa vijana 5000 kwa mwaka na kuwaunganisha vijana 10000 katika fursa za kiuchumi.

Advertisement