Taasisi za kifedha zatakiwa kuwekeza wajasiriamali wa chini, kati
Muktasari:
- Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi la benki ya Letshego Faidika, mkoani Arusha, Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, Irene Ndossi, amesema kwa kufanya hivyo itasaidia makundi hayo kukua zaidi kiuchumi
Arusha. Taasisi za kifedha nchini hasa benki,zimetakiwa kuwekeza kwa wananchi,wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaohitaji kukua kiuchumi na kukuza biashara na mitaji yao.
Aidha zimetakiwa kusogeza huduma zake kwenye maeneo ya pembezoni na vijijini ambapo hakuna huduma za kibenki ili kuwafikia wananchi kwa ukaribu na kuwapa huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya masuala ya fedha.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Juni 25, 2025 na Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude, Irene Ndossi alipomwakilisha wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki ya Letshego Faidika la jijini Arusha.
Amesema kuwa ni muhimu taasisi za kifedha hasa benki kuwekeza kwa makundi hayo na kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa na inaamini kwa kushirikiana itafanikisha ajenda ya uchumi shindani unaojumuisha watu wote.
Irene amesema Serikali inaelewa benki ni mhimili muhimu katika maendeleo ya wananchi hivyo waendelee kuongeza ujumuishaji wa fedha hasa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao ndiyo uti wa mgongo wa uchumi.
“Nasisitiza umuhimu wa kuhudumia wananchi kwa weledi uaminifu na kasi inayozingatia mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia,wananchi wanahitaji huduma bora na nafuu na zisijikite kwa wateja wa mijini bali ziwafikie waliopo pembezoni vijijini na kwenye ameneo yasiyo na huduma za kibenki za kawaida,”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Beng' Mazana, amesema mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini yanachangia kuongezeka na kukua kwa huduma za kifedha hapa nchini.
“Kwa niaba ya bodi tunashukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji yanayosaidia upanuzi wa huduma za kifedha hapa nchini.Uzinduzi wa leo ni sehemu ya upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watanzania,”
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo,Baraka Munisi,amesema lengo la kufungua tawi hilo Arusha ni kutokana na kutambua mkoa huo una mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi kupitia biashara,utalii,kilimo na masuala mengine.
“Tukiwa taasisi ya kifedha inaendeshwa kwa misingi ya uwajibikaji wa jamii,huduma zimejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya watu ya kawaida,wafanyakazi ,wakulima ,wajasiriamali, wafanyabiashara wakubwa hadi wadogo,”amesema