Tabia nchi: Yapo madhara kiafya yaletwayo na ukame

Muktasari:

  • Ukame una athari juu ya usafi kutokana na uhaba wa maji, hivyo pia kuongeza hatari ya kueneza virusi hatari na bakteria, hasa wale wanaosababisha magonjwa ya kupumua, tumbo na matumbo.

Mtandao wa https://sw.healthy-food-near-me.com/ unaeleza kuwa ukosefu wa mvua hupunguza ukuaji wa mimea hivyo kutengeneza mazingira ya uvamizi wa wadudu na magonjwa yanayoshambulia baadhi ya mazao.

Kadhalika, mavuno duni yanaweza kusababisha uhaba wa mavuno na kuongezeka kwa bei ya chakula, hivyo kuongeza hatari ya utapiamlo katika kaya zenye rasilimali chache.

Ukame una athari juu ya usafi kutokana na uhaba wa maji, hivyo pia kuongeza hatari ya kueneza virusi hatari na bakteria, hasa wale wanaosababisha magonjwa ya kupumua, tumbo na matumbo.

Mtandao huo unabainisha, “katika hali ya ukame, uwezekano wa uchafuzi wa chakula na unakuwa wa kawaida kwa kuwa kinakuwa kimebeba bakteria wakati wakulima wanamwagilia mashamba yao kwa maji yasiyofaa kwa sababu ya upungufu.”

Mtazamo huo unashabihiana kwa kiasi fulani na kauli ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dk Alex Alexander ambaye anasema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wenye shida ya mfumo wa hewa na upumuaji, hasa pumu (asthma) na nimonia (pneumonia) kwa watu wazima na watoto, yanayosababishwa na hali ya vumbi na upepo.

Anaongeza, “hii ni kawaida kutokana na upepo na vumbi, hivyo kama wilaya tumewaagiza waganga wafawidhi wa vituo vyetu vyote vya kutolea huduma ya afya wawe na dawa za magonjwa ya mfumo wa hewa na upumuaji za kutosha ili kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa.”

Kuhusu magonjwa ya mlipuko anasema, “Halmashauri ya Wilaya ya Same hakuna ugonjwa wowote wa mlipuko uliotokea kutokana na ukame uliopo sasa. Juu ya matatizo ya utapiamlo, pia hatuna visa vipya vingi (trend haijapanda) hivyo kiujumla hali ya wilaya kiafya ni shwari.

“Kuanzia Julai hadi sasa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa mfumo wa hewa, hususani nimonia, kikohozi na mafua na kama tunavyotambua, nimonia chanzo chake kikubwa ni bakteria na wanapatikana kirahisi kwenye vumbi, hivyo mazingira ya vumbi ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya mfumo wa hewa.”

Lishe na mabadiliko tabianchi

Ofisa Lishe Mtafiti wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Walbert Mgeni anasema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ukame na lishe kwa sababu upatikanaji wa vyakula hutegemea maji.

“Kunapokuwa hakuna maji basi upatikanaji wa vyakula vya baadhi ya makundi muhimu unakuwa ni tatizo. Tafiti zinaonyesha hata wakati tu wa kiangazi ni tofauti na masika,” anasema na kubainisha kwamba aina kubwa ya ukosefu wa lishe inayodhihiri ni ukondefu.

Anasema wa sasa ambako nchi inakabiliwa na upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo kutokana na mvua chache, “nina uhakika ukipima watu wengi utakumbana na tatizo la ukondefu. Hili linasababishwa na ukosefu wa vitamini A na chakula kisichotosha.”

Mgeni anasema ukame unasababisha kukosekana kwa mboga za majani za kijani na matunda ambavyo ndivyo vyanzo vikuu vya vitamini A, lakini pia ukosefu wa malisho kwa wanyama.

Tatizo hili linapoendelea kwa muda, anasema ndilo husababisha aina nyingine za utapiamlo kwa watoto kama udumavu na uzito mdogo.

Akihusisha mabadiliko ya tabianchi na lishe, Mgeni anasema yameathiri kilimo kwa kiasi kikubwa, sawia na mifumo ya vyakula kwa baadhi ya maeneo na pia lishe za watu.

Anasema maeneo ambayo kwa kawaida huathiriwa zaidi na hali hiyo ni mikoa ya kati ya nchi ingawa kwa sasa inasambaa kwenye mikoa mingi.

“Unakuta watu walizoea kulima na kula ndizi tu, au wali tu, sasa wanatakiwa kuhama na kulima mihogo, mtama na mazao mengine yanayostahimili ukame, wengi wanashindwa na hapo ndio madhara yanapotokea,” anasema.

Kwa kutambua hayo, mtaalamu huyo anashauri watu kubadili aina za kilimo na ufugaji kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na matunda kama mapapai, kufanya kilimo cha viroba na kufuga wanyama wadogowadogo kama kuku, sungura na bata ambao ni rahisi kuwahudumia.

Kila baada ya miaka minne, TFNC hufanya utafiti kuhusu lishe nchini, mara ya mwisho utafiti huo ulifanyika mnamo mwaka 2018 ambao ulionyesha kuwa viashiria vya utapiamlo vya udumavu na ukondefu vilipungua, uzito mdogo ukiongezeka.

Kwa mujibu wa matokeo ya tafiti huo, udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndicho kiashiria kikuu cha utapiamlo, umepungua kutoka asilimia 34.7 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 32 mwaka 2018.

Wakati ukondefu ukipungua kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 3.5, uzito mdogo uliongezeka hadi kufikia asilimia 14.6 kutoka asilimia 13.7.

Endapo matokeo ya utafiti huo yangefanyika na kutolewa sasa, “kwa hali ilivyo sasa ya ukame nchini na kwa mujibu wa viashiria vinavyoonekana, upo uwezekano mkubwa wa tatizo la ukondefu kuongezeka. Kwa suala la udumavu inawezekana kupungua kwa kuwa ni hali ya muda mrefu na Wizara ya Afya imefanya jitihada mbalimbali kupunguza tatizo.”

Ofisa Tatibu Zahanati ya Kwipipa, Gairo, Dk Emmanuel Kusekwa anasema usalama wa chakula ni miongoni mwa mambo yanayowasumbua wakazi hao.

Kutokana na hali ya ukame, anasema wananchi wanalazimika kuhifadhi vyakula kwa kuvikausha ili vitumike nyakati za hatari ambako anasema kunapunguza au kuondoa kabisa virutubisho, hivyo kuwasababishia magonjwa ya kusinyaa kwa ngozi.

“Ugonjwa huu unawapata zaidi wanawake, wazee na watoto wa Kwipipa, sababu wanakula vyakula vilivyokaushwa, tunapokea wagonjwa wa aina hii wengi, hasa kipindi cha kiangazi.

“Ulaji wa vyakula hivi unasababisha kukosekana kwa Vitamini E na hivyo wanapatwa na magonjwa haya mara kwa mara, wenyewe wanauita Kibandulo lakini kitaalamu unaitwa Isizima,” anasema.

Mbali na ugonjwa huo, anasema mwingine ni kuhisi maumivu ya tumbo mithili ya kuungua na wengi wanapungukiwa nguvu ingawa hakuna madhara zaidi.

Kuthibitisha hayo, mkazi wa Kijiji cha Kwipipa wilayani Gairo, Regina Bisoweto anasema katika kipindi cha kiangazi wanakabiliwa na kunyauka kwa ngozi na maumivu ya tumbo.

“Kujinusuru na ugonjwa huu tunashauriwa tutumie lishe kwa nguvu, tunywe maziwa wakati hayapo maana kuna jua kali maziwa hayatoki,” anasema.