Tabia tano zitakazokuweka karibu na mwanao

Wazazi wengi kama sio wote, hutamani kuwa karibu na watoto wao. Tafiti za malezi zinabainisha kuwa ukaribu huu imara unaogusa mioyo ya watoto huweka mazingira ya kuwajengea watoto tabia njema.

Moja ya sababu zinazofanya watoto wakose nidhamu kwa wazazi wao, ni ule umbali wanaouona kati yao na wazazi. Mtoto anayejisikia kuwa mbali na mzazi wake si tu hujikuta akienda kinyume na matarajio ya mzazi lakini pia huwa si mwepesi kutoa ushirikiano.

Utovu huu wa nidhamu, tafiti zinasema, mara nyingi ni mwitikio wa kitoto unaolenga kutafuta ukaribu na wazazi. Wakati wazazi tunapokuwa na watoto tunatumia muda mwingi kukemea, kulalamika, kufoka, kukumbusha na kuelekeza, tunasahau watoto hutamani kuwa na sisi kwa minajili ya kujenga uhusiano wa karibu.

Katika makala haya tunapendekeza tabia tano unazoweza kujizoeza kila siku zinazoweza kuimarisha mahusiano yako ya karibu na mwanao.

Patikana

Kama wazazi tunaowajibika, tunayo mambo mengi yanayochukua muda wetu mwingi. Mengi ya mambo haya, kwa hakika, yanalenga kuwajengea watoto hao hao misingi bora ya maisha yao ya baadae.

Hata hivyo ni muhimu kuelewa kuwa watoto wanahitaji kuwa na muda na sisi hata kama hawana ujasiri wa kutuambia.

Katika kuonyesha umuhimu wa kupatikana, tafiti za malezi zinasema, kwa kawaida, mtoto anahitaji takribani majuma 900 katika utoto wake akiwa kwenye mikono ya wazazi wake kabla hajaondoka nyumbani kwenda kujitegemea.

Muda huu, ambao ni sawa na miaka 17, ni fursa ya uwekezaji kwetu wazazi katika kuhakikisha mtoto anauelewa utamaduni wa familia kabla hajakutana na watu wengine huko duniani.

Maana yake ni kwamba ni muhimu kwako mzazi kufanya kila unaloweza kutenga muda mfupi kila siku uzungumze na mwanao. Watoto wanathamini sana nyakati kama hizi wanapokuwa karibu na wazazi wao. Kama unao watoto zaidi ya mmoja, jitahidi kupata muda na kila mtoto mzungumze kibinafsi.

Jaribu jambo hili: kila unapokuwa na mtoto acha shughuli zote unazofanya na upatikane kwa asilimia 100. Kuwa na mtoto kimwili, kiakili, kisaikolojia badala ya kuacha mawazo yako yahame.

Pia, epuka kutawala mazungumzo. Mpe nafasi akuambie siku yake imeendaje. Uliza mambo ya shule, mambo aliyokutana nayo mchana kutwa na mruhusu aamue aina ya shughuli mnazoweza kuzifanya mkiwa pamoja.

Kumkumbatia

Kisaikolojia kukumbatiwa ni hitaji muhimu la kila mwanadamu timamu. Unapokumbatiwa, kwa kawaida, unajisikia kuwa karibu na aliyekukumbatia.

Jenga tabia ya kumkumbatia mwanao kila siku asubuhi na ikiwezekana kila anapokuaga kwenda kulala. Pia mkumbatie unapomuaga kwenda mahali, mkumbatie unapokutana naye baada ya muda na mkumbatie anapokuwa kwenye nyakati zinazohitaji faraja.

Unapomkumbatia mtoto mpapase kichwa chake taratibu. Tumia viganja vyako ‘kumkanda kanda’ mabega yake na sehemu za mgongoni. Mtazame machoni ukimwonesha tabasamu la upendo. Ukifanya hivi utajenga uhusiano wa karibu naye.

Jambo la kuzingatia ni kwamba kwa watoto wakubwa kidogo inaweza kuwa kazi kubwa kupokea mazoea haya mapya. Usikate tamaa mapema. Kadri utakavyoonekana kumaanisha ndivyo itakavyokuwa rahisi kupokelewa.

Kucheza

Michezo ina nafasi kubwa ya kukuweka karibu na mtoto. Kuna mambo mtalazimika kuyafanya mnapocheza na yataweka kumbukumbu ya kudumu kwenye ufahamu wa mtoto.

Kwenye michezo, kwa mfano, mtacheka, mtazungumza na mtataniana. Mambo haya hupunguza ule umbali wa kisaikolojia kati yenu. Ucheshi na mazungumzo ya mara kwa mara hufanya mzoeane na hiyo inasaidia kujenga mahusiano yenu.

Unapocheza na mwanao, hakikisha unafahamu anapenda mchezo gani. Huna sababu ya kumlazimisha mtoto kupenda kile unachokipenda wewe. Ungana naye kwenye michezo anayoipenda yeye.

Pia, ni vyema kuhakikisha unaachana na shughuli nyingine zinazoweza kukuondolea uzingativu kwa mwanao. Vitu kama simu, kufanya mazungumzo na watu wengine, kusikiliza muziki na kutumia kompyuta wakati wa michezo na watoto hutuma ujumbe kuwa hujalivya kutosha.

Mruhusu aoneshe hisia

Katika utamaduni wetu tunafundishwa kuficha hisia. Tunajisikia fahari watu wanapotuchukulia kama watu tusio na hisia. Kwa sababu hii unaweza kukutana na mtu mwenye ghadhabu lakini anaigiza kuwa na furaha.

Kisaikolojia tabia hii ya kuficha hisia haina tija. Mtu asiyeonesha hisia zake, mara nyingi, huugulia maumivu ndani kwa ndani kwa hofu ya kuhukumiwa endapo atazionyesha.

Unapohusiana na mwanao mpe nafasi ya kuonyesha hisia alizonazo. Ikiwa ana hisira, usimzuie kuonyesha hasira zake. Mbali na kumsaidia kujitibu mwenyewe, kuonesha hasira kunamsaidia kuwa mkweli wa hisia zake.

Sambamba na kumruhusu kuonyesha hisia zake, unahitaji kuwa mfano wa mtu anayemudu hisia. Unapokasirishwa na makosa yake, epuka kulipuka bila kufikiri. Jipe muda wa kutulia na shughulikia tatizo hasira zikishapoa. Kwa namna hii unamfundisha mtoto tabia ya kumudu hisia zake.

Sikiliza na muelewe

Kwa kawaida, uhusiano na mtu yeyote huanzia kwenye uwezo wa kumsikiliza. Usipokuwa na uwezo wa kusikiliza kwa makini hutaweza kuaminiwa na watu wengi.

Mtoto anapokueleza jambo, onyesha kufuatilia. Itikia kwa ishara ya mwili na sauti, ‘Aisee! Kweli? Ilikuwaje? Hebu eleza zaidi nielewe ilivyokuwa!” Maneno kama haya yanamtia moyo mtoto na yanamfanya ajiamini anapokuwa na wewe.

Jifunze kutazama mambo kwa macho ya mwanao. Heshimu yale anayokueleza bila kurukia kumkosoa, kumrekebisha, kumwelekeza. Hata kama anakosea, mpe nafasi aeleze kwanza. Ikiwa ni lazima kumrekebisha, fanya hivyo baada ya kumwonyesha kuwa umemsikiliza na umemwelewa.

Wakati mwingine tunajikuta tukiwaadhibu watoto kwa sababu tu pengine hatujaweza kuelewa wanafikiri nini. Tunataka wafikiri kama watu wazima, wafanye kama watu wazima na waamue kama watu wazima.

Mpe mtoto nafasi ya kuwa mtoto. Huna sababu ya kuadhibu kila kosa. Kukosea ni sehemu ya makuzi yake. Wakati mwingine tukiweza kuelewa kwa nini mtoto amelifanya kile tunachoona ni kosa tunaweza kumrekebisha vizuri zaidi.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com

Twitter: @bwaya