Tabora kuwabaini ‘wachakachuaji' maziwa kwa kifaa maalum

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian (katikati) akizungumzia kuhusu wiki ya Maziwa inayotarajia kufanyika Kitaifa  mkoani Tabora kuanzia Mei 29 hadi Juni 1, 2023.Kulia ni kaimu Katibu Tawala wa Uchumi na Uwekezaji, Modest Kaijage na kushoto ni Ofisa Uhusiano wa Umma Bodi ya Maziwa Tanzania.Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

Wastani wa kitaifa wa unywaji wa maziwa kwa mtu mmoja ni lita 62 kwa mwaka huku kimataifa ikiwa ni lita 200.

Tabora. Mkoa wa Tabora utaanza kutumia kifaa maalum cha kupima maziwa kama yameongezwa maji ili kuwabaini wafanyabiashara wanao yachanganyia maji kwa lengo la kujipatia kipato zaidi.

Akizungumzia maadhimisho ya wiki ya maziwa leo Ijumaa Mei 26, 2023 yanayotarajia kufanyikia mkoani Tabora Mei 29, Mkuu wa Mkoa huo, Dk Batilda Burian amesema wapo baadhi ya wafanyabiashara ya maziwa wanaoongeza maji jambo ambalo sio zuri.

“Kuongeza maji kumesababisha wengi kutopenda kunywa maziwa katika mkoa wetu,”amesema

Ametaka wafanyabiashara hiyo kuacha kuchanganya na maji akidai  watachukuliwa hatua za kisheria huku, akiahidi Serikali itaweka kituo cha kukusanyia maziwa ambacho kitakuwa na manufaa makubwa.

Katika hatua nyingine, amewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa ya wiki hiyo ambayo itazinduliwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde na kufungwa na Waziri wake, Abdallah Ulega.

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uwekezaji Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Ofisa Kilimo wa Mkoa huo, Modest Kaijage amesema vifaa vinavyotumiwa na wauza maziwa sio vizuri kwani ni vya plastiki na sio salama.

Amesema wakaguzi wa maziwa watateuliwa na maziwa kupimwa ili wananchi wapate bora kwa manufaa ya afya zao.

Ofisa Uhusiano wa Umma Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Tajiri Kihemba amesema shughuli mbalimbali zitafanyika katika wiki hiyo ikiwemo kugawa maziwa katika baadhi ya Taasisi zikiwemo shule.