Tahadhari virusi vipya vya corona

Serikali yaongeza msisitizo dhidi ya corona

Muktasari:

  • Mwongozo mpya wa corona waweka mkazo viwanja vya ndege, madaktari watoa angalizo

Wakati Serikali ikiimarisha ukaguzi, upimaji na ulinzi dhidi ya virusi vya corona katika viwanja vya ndege na mipakani, wataalamu wa afya wametoa angalizo kuhusu tabia ya virusi vipya vilivyoibuka nchini India.

 Mjadala kuhusu uwezekano wa kurejea upya kwa maambukizo ya virusi vya corona umeanza kujitokeza, hasa kutokana na uhusiano wa karibu baina ya Watanzania wenye asili ya India ambao huenda nchini humo na kurejea nchini mara kwa mara.

 Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shadrack Mwaibambe ametoa angalizo kwa Serikali kuhusu virusi hivyo.

Amesema kuna watu kipimo kinaweza kuonyesha hawana maambukizo wakati wana dalili zote za corona na kwamba India watu wameugua hata kupoteza maisha lakini vipimo vilionyesha hawakuwa na maambukizo.

“Hili ni angalizo muhimu sana kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari kama inavyoshauriwa, vaa barakoa, epuka mikusanyiko kadri uwezavyo, hali siyo salama.

Tusubiri ripoti ya tume iliyoundwa na Rais SHassan ili tujue mwelekeo wa nchi juu ya njia nyingine za kujikinga,” alisema Dk Mwaibambe.

Aidha Mwaibambe alisema MAT inaunga mkono hatua ya Serikali kudhibiti uingiaji wa wageni kutoka nje ya nchi, kwani Tanzania imetumika sana kama kimbilio kwa kigezo cha utalii.

 “Katika kipindi hiki, wasafiri wanapenda kwenda nchi zinazoruhusu watu kuingia kiholela, hivyo vigezo ambavyo Serikali imeweka ni vizuri kwa kulinda raia wake dhidi ya maambukizo ya Covid 19,” alisema.

Serikali yasitisha safari za India Jana Serikali ilisitisha safari za ndege zote kutoka India kuingia nchini na kuzuia zile zinazofanya safari za huko, kufuatia aina mpya ya virusi vya Covid 19 inayoongeza maambukizo na vifo nchini humo.

Katibu mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Profesa Abel Makubi amesema hayo kupitia mwongozo mpya wa wasafiri namba 7 siku moja baada ya kutoa mwongozo namba 6, ikiwa ni maboresho ya kulinda mipaka ya nchi.

 “Tumezifungia ndege hizi mpaka pale tutakapotangaza vinginevyo na ndege zitakazoruhusiwa ni zile za mizigo, lakini wahudumu hawataruhusiwa kushuka, ndege zinazobeba dawa, za kidiplomasia na misaada tu ndizo zitaruhusiwa kutua,” alisema.

 Profesa Makubi alisema Watanzania wanaowasili kutoka nchi hizo wakiwamo wanafunzi, walioenda kibiashara au kwa matibabu watatakiwa kuzingatia masharti yaliyowekwa.

“Wasafiri wote wanaorejea kutoka India siku 14 nyuma wanatakiwa kupimwa kipimo cha Covid-19 na kabla ya kurejea wapime saa 72 na wakirejea watapimwa tena na watatakiwa kukaa karantini kwa siku 14 kwa gharama zao.

“Watakaowasili watatakiwa kuchagua mahali pa kukaa kwa siku 14 kupitia nafasi zilizopo uwanja wa ndege au kuchagua katika wavuti wa wizara (https:// www.moh.go.tz/en/) kuna sehemu zilizopendekezwa na Serikali,” alisema.

Amesema wasafiri watakaowasili kutoka India wataruhusiwa kujitenga katika nyumba zao kwa siku 14 ili kunusuru maambukizo kwa kufuata masharti ya Wizara ya Afya.

Profesa Makubi alisema wasafiri wote au wanaorejea watatakiwa kujaza fomu maalumu kabla ya kuwasili nchini kulingana na maelekezo yaliyowekwa na yeyote atakayethibitika kuwa na viashiria atapimwa na watakaoumwa watatibiwa katika vituo vilivyotengwa na Serikali kwa gharama zao wenyewe.

“Wasafiri wote wanatakiwa kujaza fomu maalumu iliyopo mtandao wa wizara ambao ni https: afyamsafiri.moh.go.tz saa 24 kabla ya kuwasili Tanzania na msafiri yeyote lazima aambatanishe cheti kinachoonyesha hana maambukizo ambacho kinatakiwa kionyeshe amepimwa coronasaa 72 kabla ya kuwasili,” alisema.