Tahasusi 49 zaongezwa kwa wahitimu kidato cha nne

Muktasari:

  • Serikali imefungua pazia kwa wahitimu wa kidato cha nne wa mwaka 2023 kubadilisha tahususi zao ili kufanya machaguo sahihi ya masomo yao ya juu, pia imeongeza tahasusi kutoka 49 kutoka 16 za awali hadi 65.

Dar es Salaam. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetoa fursa kwa wahitimu wa kidato cha nne wa mwaka 2023 kubadilisha machaguo yao ya masomo wanayotarajia kusoma wanapoendelea na elimu ya juu baada ya kuongeza tahasusi 49.

Tamisemi imetoa fursa hiyo ikiwa imezingatia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la mwaka 2023 na mitalaa ya elimu kwa kidato cha tano, inayoelekeza kuanza utekelezaji wa mafunzo ya elimu ya amali.

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliyetangaza fursa hiyo leo Machi 20, 2024 amesema, “utekelezaji huo umehusisha uanzishaji wa tahasusi mpya 49, kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia tahasusi 65.”

Amesema mabadiliko hayo yatagusa tahasusi ‘kombinesheni’ za kidato cha tano na kozi za vyuo vya ualimu, vyuo vya kati na elimu ya ufundi kwenye mfumo wa kieletroniki ili kufanya marekebisho ya machaguo kulingana na ufaulu walioupata.

Waziri Mchengerwa amesema,”mchakato huu unaoanza leo Machi 20, 2024 utahitimishwa  Aprili 30, 2024 utatoa fursa ya wanafunzi kufanya mabadiliko ya machaguo, tahususi au kozi kwa njia mtandao.

“Baada ya kufanyamarekebisho haya, kanzidata hiyo ndio itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za kidato cha tano na kozi mbalimbali katika vyuo vya kati na elimu ya ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo,” amesema.

Waziri Mchengerwa amesema Serikali imeshakamilisha mchakato wa awali wa kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye fomu za uchaguzi za wanafunzi, kama walivyozijaza wakiwa shuleni.

Amesema mabadiliko ya sera ya elimu ya mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 na mitaala ya elimu kwa kidato cha tano yameanza kutekelezwa ikiwamo uanzishwaji wa tahasusi mpya 49 kutoka 16 zilizokuwapo awali.

“Ukweli ni kwamba wakati wa ujazaji wa fomu za machaguo ya awali tahasusi mpya 49 hazikuwepo kwenye orodha ya machaguo na pia matokeo ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne hayakuwa yametoka kumwezesha mwanafunzi kuwa na machaguo mazuri zaidi kulingana na ufaulu wake.

“Hivyo, mchakato huu utatoa fursa zaidi wanafunzi kuongeza machaguo na kufanya machaguo mapya ya tahasusi na kozi, niwasihi wazazi na walezi kushiriki katika suala hili ili kuwashauri watoto kufanya uamuzi sahihi kulingana ufaulu wao,” amesema Mchengerwa.

Pia, amesema tahasusi mpya zitakazoanza kutumika Julai mwaka huu zipo katika makundi saba ambayo ni tahasusi ya sayansi ya jamii, lugha, masomo ya biashara, tahasusi za sayansi, michezo, sanaa na tahasusi za elimu ya dini.

Kufuatia tangazo hilo, mdau wa elimu, Dk Aviti Mushi amesema hiyo ni hatua nzuri iliyofanywa na Tamisemi ya kuwapa fursa wanafunzi kufanya machaguo sambamba na kuongeza tahususi, ingawa ana shaka na kubadilisha tahasusi kulingana na ufaulu.

“Tunataka kujenga jamii yenye watu wenye weledi na kufanya kazi, lazima tuhakikishe kila mtu anakuwa na kiwango cha kuanzia ili kubadilisha tahasusi.

“Nimesema ufaulu kwa sababu inaweza kujitokeza kuwa labda taalumu hii ipo hivi basi ufaulu wake utakuwa juu, jambo litakalowanyima fursa wengine ambao wangeweza kufanya vitu vizuri endapo wangepata nafasi ya kufanya kufanya mabadiliko ya tahasusi,”amesema Dk Mushi ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM).

Dk Mushi ameipongeza Tamisemi kwa kuongeza tahasusi kwa sababu inapanua wigo wa vijana kujifunza taaluma mbalimbali, akisema ndivyo maisha yalivyo, si wote ni wahandisi wengine ni madaktari.

Mdau mwingine, Suzan Lyimo amesema wanafunzi wengi walikuwa wanabanwa na tahasusi kwa sababu walikuwa wanajaza kabla ya matokeo ya mtihani.

“Unakuta mtu amejaza kabla ya matokeo kutoka, yakitoka unajikuta yale uliyojaza hukufaulu vizuri, lakini kwa vile sasa matokeo wanayajua na tahasusi zimeongezeka watafanya machaguoa sahihi na uwanda utakuwa mpana.

“Naona ni jambo jema hata huko tuendako iwe hivyo, watu wachague tahasusi baada ya kufanya mtihani, kichotakiwa kuwekwa kwa utaratibu mzuri, ndio maana shule zingine zina nafasi lakini wanafunzi hakuna kwa sababu tahasusi hazijakaa sawa,” alisema Lyimo.