Takukuru: Hata kwenye kilimo kuna mianya ya rushwa

Saturday August 06 2022
By Tumaini Msowoya

Mbeya.  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) imesema hata kwenye kilimo kuna vitendo vya rushwa vinavyoweza kukwamisha jitihada za kukuza sekta hiyo hadi kufikia mkakati wa 10/30.

 Ofisa uchunguzi kutoka Takukuru Makao Makuu, John Shija ametaja baadhi ya maeneo yenye mianya ya rushwa kuwa ni kwenye ugawaji wa pembejeo za kilimo na uuzaji wa mazao hasa kupitia vyama vya ushirika kutokana na baadhi ya viongozi kutokuwa waaminifu.

Akizungumza kwenye maonyesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale, Jijini Mbeya Shija amewataka wakulima kutoa taarifa ikiwa wataona kuna viashiria vya rushwa.

Alisema pamoja na elimu inayoendelea kutolewa kuhusu rushwa, bado tatizo hilo linaendelea jambo ambalo hawawezi kulifumbia macho.

“Tumeona hata kwenye sekta ya kilimo kuna mianya ya rushwa, tukianzia katika ugawaji wa pembejeo za kilimo, kuna watu wanatumia fursa hiyo kujinufaisha wenyewe, tunaendelea kutoa elimu kwa wataalamu wetu wazingatie miiko na maadili ya kazi zao,” amesema Shija

Amesema pia ipo mianya ya rushwa kwenye uuzwaji wa mazao ya kilimo kutokana na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika kutokuwa waaminifu na hivyo kuwaumiza wakulima.

Advertisement


Kutokana na hali hiyo, amewataka wakulima kutofumbia macho vitendo vya rushwa na badala yake kutoa taarifa Takukuru ili hatua za haraka zichukuliwe.

“Sekta hii ya kilimo ina miradi mikubwa, Serikali imewekeza fedha nyingi hivyo tusipokuwa na watendaji waaminifu ni hatari kwa sababu wanaweza kujinufaisha. Mnapoona viashiria vya rushwa toeni taarifa,” amesema Shija.

Kwa upande wao baadhi wananchi na wakulima walisema vitendo vya rushwa vipo katika taasisi zote na kwamba ipo haja ya kuendelea kutoa elimu juu ya namna ya kupambana nalo.

“Wakati mwingine mtu unalazimika utoe rushwa ili upate huduma kwa haraka ukihofia milolongo mirefu, fikiria mazao yapo shambani na nahitaji pembejeo, nazungushwa wee sasa ili mazao yasiharibike mtu anaamua kutoa rushwa. Tunahitaji elimu lakini Takukuru watufikie,” amesema Joshua Mulinga.

Advertisement