Takukuru kuchunguza mradi Bweni la shule uliogharimu Sh298 milioni

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Mussa Chaulo akizungumza leo Aprili 23, 2024 na waandishi wa habari ( hawapo pichani) mjini Moshi.

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imeanza uchunguzi wa mradi wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya wasichana Machame, iliyopo Wilaya ya Hai, ambao tayari umegharimu zaidi ya Sh298 milioni.

Moshi. Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imeanza uchunguzi wa mradi wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya wasichana Machame, iliyopo Wilaya ya Hai, ambao tayari umegharimu zaidi ya Sh298 milioni.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 23, 2024 na Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Mussa Chaulo wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

Chaulo amesema wamefanya ufuatiliaji wa fedha za umma katika miradi ya maendeleo 40, yenye thamani ya zaidi ya Sh23.26 bilioni katika sekta ya afya, elimu, maji na ujenzi.

Amesema katika miradi hiyo, mradi mmoja wa ujenzi wa bweni la Shule ya Machame umeanza kufanyiwa uchunguzi baada ya fedha zilizotolewa Sh260 milioni kumalizika na kuongezwa  nyingine, Sh38 milioni ambazo pia zimeshindwa kuukamilisha.

Amesema katika kipindi hicho chambuzi sita zilifanyika ili kubaini iwapo kuna mianya ya rushwa katika mifumo mbalimbali kwa lengo la kuweka mikakati ya kuidhibiti.

Hata hivyo, amesema chambuzi tano bado zinaendelea kufanyiwa kazi, huku moja inayohusu usimamizi na uendeshaji wa kituo cha utalii cha chemka (Chemka hot spring) kilichopo Wilaya ya Hai, ukibaini hakuna sheria ndogo inayoruhusu halmashauri husika kukusanya mapato ndani ya chanzo hicho.

 Malalamiko yaliyopokelewa

Chaulo amesema katika kipindi hicho cha miezi mitatu taasisi hiyo imepokea malalamiko 122, ambapo 74 yalihusu makosa ya rushwa na 48 hayakuwa na mahusiano yoyote na utoaji au upokeaji wa rushwa, ambapo uchunguzi mbalimbali unaendelea kuhusiana na yanayohusiana na rushwa.

Akitoa ufafanuzi wa taarifa hiyo kisekta,  Chaulo amesema kati ya malalamiko hayo yaliyohusu Tamisemi yalikuwa 43, binafsi 13,elimu 12, ujenzi 11,ulinzi 11, sekta ya afya  manane, ardhi sita, Tasaf moja, mahakama manne, siasa mawili, ushirika sita, nishati mawili, Rita mawili na taasisi za fedha mmoja.

Amesema katika kipindi hicho, kesi tatu mpya zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali mkoani Kilimanjaro na kufanya jumla ya kesi zinazohusiana na rushwa zinazoendelea mkaoni humo kuwa 29, ambapo kati ya hizo kubwa  ni moja (grand corruption) huku katika  kipindi hicho Jamhuri ilishinda kesi tatu.

Akizungumzia kituo cha utalii cha Chemka Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la Pangani, Segule Segule amesema moja ya majukumu ya bodi hiyo ni kuratibu rasilimali maji, kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji na kukiri Halmashauri ya Hai na wadau wengine kutumia chanzo hicho bila kuwa na kibali.

“Tukiri tu kwamba zipo nyakati aidha kwa sababu za uelewa, watu wanachelewa kuomba vibali, niwashukuru Takukuru wamekuwa jicho la kutukumbusha kuhakikisha utaratibu unaopaswa kufuatwa, na sisi tumechukua hatua za kuweka alama za mipaka kuainisha mwisho wa eneo la chanzo cha maji na kuweka mapango,” amesema.