Takukuru ‘kukomaa’ na Polisi waliofungwa miaka 20 kwa kuchukua Sh73 milioni za msaidizi wa Mwalimu Nyerere

Muktasari:

  • Wiki mbili baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwatia hatiani na kuwahukumu waliokuwa askari Polisi watatu kifungo cha miaka 20 jela na kuwaachia wengine, Takukuru imesema inafuatilia hukumu hiyo ili kuona uwezekano wa kukata rufaa kumwezesha mlalamikaji kulipwa fedha zake.

Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa, imesema inasubiri kupokea nakala ya hukumu iliyowatia hatiani na kuwahukumu waliokuwa askari Polisi watatu kifungo cha miaka 20 jela, ili kuona uwezekano wa kukata rufaa.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 16/2023, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliwahukumu waliokuwa askari Polisi watatu kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kutumia vibaya madaraka yao na kumfanyia upekuzi haramu, Profesa Justin Maeda.

Profesa Maeda, alikuwa ni mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa masuala ya uchumi wa Rais wa awamu ya kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Ilidaiwa kuwa Machi 19, 2021, washitakiwa walikwenda nyumbani kwa Profesa Maeda na kufanya upekuzi na kudai wamekuta meno ya tembo kwenye shamba lake, kisha kudai fedha hizo ili wasimchukulie hatua za kisheria.

Shitaka lingine lilikuwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh73 milioni kati ya 100 walizodaiwa kuomba na kosa la tatu ni kusaidia kutenda kosa lililokuwa likimkabili raia pekee katika kesi hiyo, Wilfred Mollel.

Hakimu Regina Oyier aliyetoa hukumu hiyo, alisema shitaka la kuomba na kupokea rushwa na kosa la kusaidia kutenda kosa la jinai lililokuwa likimkabili Mollel pekee, halikuthibitika mahakamani.

Aliwaachia huru askari wanne pamoja na Mollel kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kwa viwango vinavyokubalika kisheria.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi wiki iliyopita, Profesa Maeda alisema anachohitaji ni kurejeshewa fedha zake zaidi ya Sh70 milioni, akieleza kushanagazwa na hukumu ya kuwafunga jela bila kuzungumzia hatima ya fedha zake ambazo zilichukuliwa na askari hao.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Januari 13, 2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema kwa sasa wanasubiri nakala ya hukumu hiyo ndipo waone hatua wanazoweza kuchukua ikiwemo kukata rufaa au kumshauri ni vipi mlalamikaji anaweza kupata  fedha zake.

“Huwezi ukawa na uamuzi mpaka upate nakala ya hukumu, ikishapitiwa vizuri ndipo tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusema tutachukua hatua gani.

“Unapokuwa na nakala unapitia kila sentensi na kusema huu uamuzi kuna mahala una shida au tukate rufaa,” amesema.

Amesema ikiwa hawakukutwa na hatia kwenye kosa la rushwa ambalo waliwashitaki nalo, watakapoisoma hukumu hiyo watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kumshauri mtu huyo ambaye tukio linamhusu.

 “Mtu anapoona kuna haki yake mahali amekosa basi milango ni mingi, sheria imeweka hiyo fursa,” amesema.