Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takukuru yakamilisha uchunguzi wizi wa mifuko 600 ya saruji

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Anthony Gang'olo akizungumza na waandishi wa habari juu ya utendaji kazi wa taasisi hiyo katika robo ya kwanza kwa mwama 2023/24. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Takukuru Mkoa wa Mara inasubiri kibali kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili kuwafukisha mahakamani watuhumiwa wa wizi wa mifuko zaidi ya 600 ya saruji kwenye mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Mkoa wa Mara.

Musoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara imekamilisha uchunguzi juu ya tuhuma za wizi wa mifuko zaidi ya 600 ya saruji kwenye mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Mkoa wa Mara.

Kufuatia kukamilika kwa uchunguzi huo taasisi hiyo inasubiri  kibali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Ijumaa Novemba17, 2023; Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Anthony Gang'olo amesema baada ya kupokea taarifa za wizi wa mifuko hiyo ofisi yake ilianza uchunguzi mara moja ili kubaini ukweli.

Hata hivyo Gang'olo hakuwa tayari kutaja majina wala idadi ya watuhumiwa kwa madai kuwa majina hayo yatajulikana baada ya watuhumiwa kufikishwa  mahakamani.

"Kikubwa kwasasa ni kwamba tumekamilisha uchunguzi wetu na kuna watuhumiwa tunao, kuhusu idadi, majina na kazi zao hebu tusubiri kwanza tupate kibali na siku wakifikishwa mahakamani kila kitu kitajulikana,” amesema Gang'olo

Mifuko hiyo ya saruji inadaiwa kuibiwa kutoka katika eneo la mradi na kupatikana ikiwa imehifadhiwa nyumbani kwa mkazi wa kijiji cha Karukekere umbali wa zaidi ya kilomita 15 kutoka katika eneo la mradi.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano alisema Serikali inatekeleza mradi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya mkoa katika kijiji cha Bulamba wilayani humo kwa gharama ya zaidi ya Sh4 bilioni ambapo hadi sasa Sh3 bilioni zimetolewa.

Akizungumza katika eneo la tukio, mkuu huyo wa wilaya alisema wanaamini wizi huo umefanywa kwa ushirkiano baina ya watendaji wa halmashauri ya Bunda vijijini na watu wengine ambapo aliagiza uchunguzi kuanza mara moja.

Katika hatua nyingine, Takukuru imebaini uwepo wa dosari kwenye miradi mitatu ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh850 milioni  katika wilaya za Butiama, Rorya na Serengeti.

Gang'olo amesema dosari hizo zimebainika kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu kufuatia ufutiliaji wa miradi 30 yenye thamani ya zaidi ya Sh12.4 bilioni uliofanywa na ofisi yake.

"Miradi yenye kasoro ilikuwa kwenye sekta za elimu na afya ambapo tulibaini mambo mengi ikiwemo uwepo wa matofali 800 yenye thamani ya zaidi ya Sh1.6 milioni zenye ubora chini ya kiwango kwenye mradi wa ujenzi wa miundombinu katika shule ya Sekondari Buturi,”

“Pia tulibaini ujenzi wa chini ya kiwango na ununuzi wa vifaa vya ujenzi usiozingatia mahitaji pamoja na mambo mengine katika mradi hiyo,"amesema

Amedai kutokana na hali hiyo wameagiza marekebisho kufanyika ili miradi hiyo iweze kutekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha na  taratibu huku uchunguzi pia ukiwa umeanza kutokana na kuwepo viashiria vya rushwa.