Takukuru yabaini ukosefu wa maji kwenye huduma za kijamii

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Simiyu, Aron Misanga akizungumza na wandishi wa habari. Licha na Samirah Yusuph.

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa na Takukuru imebaini kuwa hakuna vituo vya maji katika maeneo ya huduma za kijamii kikiwemo kituo kikuu cha mabasi cha Mkoa wa Simiyu (Somanda) na soko kuu la mjini Bariadi.

Simiyu. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Simiyu, imebaini ufanisi mdogo katika utendaji kazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mji wa Bariadi (Baruwasa) wakati ikifanya uchambuzi wa mfumo ili kubaini mianya ya rushwa kwenye upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya huduma za kijamii.

Akitoa taarifa ya utendaji kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2023 leo Novemba 10, 2023 Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Simiyu, Aron Misanga amesema suala la kukosa maji katika maeneo ya huduma za kijamii linapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

"Maeneo yote haya tunayajua umuhimu wake ni sehemu zinazotoa huduma mbalimbali za kijamii kama vyakula kwahiyo kukosa maji sio jambo jema, stendi kuu ya Somanda kunawatu wanapanda wengine wanashuka vile vile kunawale ambao wapo muda wote; mawakala wa mabasi, wafanyabiashara na wapiga debe wanahitaji huduma ya maji," amesema Misanga

Ameongeza kuwa licha ya hivyo, pia hakuna ushirikiano kati ya Serikali za mitaa, Tarura, Tanroad na mamlaka hiyo katika uwekekaji wa miundombinu ya maji hali inayosababisha kuharibiwa kwa miundombinu ya maji wakati wa uwekaji wa miundombinu mingine.

Katika hatua nyingine, Misanga amesema taasisi hiyo ilifuatilia miradi 24 ya maendeleo yenye thamani ya Sh8.8 bilioni kwa lengo la kudhibiti ubadhirifu na kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha abapo hata hivyo ilibaini mapungufu katika maeneo ya ujenzi, usimamizi na manunuzi.

“Uchunguzi umeanza baada ya kugundua ukiukwaji wa taratibu za manunuzi katika mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi Nyangaka halmashauri ya mji wa Bariadi ambao ni mradi wa boost uliogharimu Sh543 milioni," amesema Misanga

Ameongeza kuwa wamebaini ubadhirifu katika uwasilishaji wa makato ya kodi ya zuio kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa zaidi ya Sh50 milioni kutoka Halmashauri zote sita za mkoa wa Simiyu.