Mkuu wa Takukuru Njombe afichua chanzo wizi vifaa vya miradi
Muktasari:
- Wasimamizi wa miradi mkoani Njombe watakiwa kuwalipa makandarasi kwa wakati.
Njombe. Wasimamizi wa miradi ya serikali mkoani Njombe wametakiwa kuwalipa makandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kwa wakati kwani kushindwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha wizi wa vifaa kwenye miradi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Njombe, Kassim Ephrem wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.
Amesema makandarasi wanapofanya kazi za serikali na kuacha shughuli zingine na kushindwa kulipwa kwa wakati kunaweza kuchangia wizi wa vifaa vya miradi katika siku zijazo.
"Mfano mafundi wanalalamika hatujalipwa malipo yetu tunaamini kabisa kitendo cha fundi kuacha kazi zake na kuja kufanya kazi za serikali halafu hamjamlipa inamkatisha tamaa na hayo yanaashiria huko tuendapo hata wizi wa vifaa kwenye mradi," amesema Ephrem.
Amesema kama serikali imetuma fedha kwenye mradi hakuna sababu ya kushindwa kuwalipa mafundi hao ili wafanye kazi hiyo kwa viwango na uaminifu mkubwa.
Amesema malipo hayo yafanyike baada ya tathmini kufanyika kuwa kazi iliyofanyika inaenda na thamani ya fedha inayotakiwa kulipwa mafundi hao.
Amesema kama fedha hiyo haipo ni vizuri ikatumika lugha nzuri kuwaambia mafundi hao ili waelewa kuliko kutoa maneno ambayo yatawakatisha tamaa.
Amesema katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai mpaka Septemba mwaka huu taasisi hiyo imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 39 yenye thamani ya shilingi 36.3.
Amesema kati ya miradi hiyo 31 ni kutoka sekta ya elimu, 5 kwenye sekta ya afya na 3 kwenye sekta ya maji ambayo kwa pamoja inagharimu kiasi hicho cha fedha.
Amesema miradi kumi na mbili kati ya hiyo ambayo thamani yake ni Sh12. 1 bilioni ilibainika kuwa na mapungufu na hatua mbalimbali zimechukuliwa kurekebisha mapungufu hayo.
Amewataka makandarasi mkoani hapa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ili iweze kukamilika kwa wakati kabla ya mvua kuchanganya.
Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Wanging'ombe, Scholastica Assey amesema ili kuendelea kupambana na rushwa wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano pindi wanapotakiwa kutoa ushahidi mahakamani.
"Kwa zile taarifa ambazo mtu unatakiwa kusimsma mahakamani wawe tayari kusimama mahakamani kwa kuwa kesi hiyo ni ya Jamhuri usipotoa ushahidi kesi hiyo haina maana," amesema Assey.