Takukuru yashtukia upigaji Sh250 milioni ujenzi wa madarasa
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Elisante Mashauri.
Muktasari:
- Takukuru Mkoa wa Mtwara yazuia Sh250 milioni zilizolipwa kinyemela katika akaunti ya mzabuni Mubba General Supplie kutoka katika akaunti ya shule ya sekondari Mustapha sabodo fedha ambazo zilitakiwa kununua vifaa vya ujenzi wa vyoo, madarasa na mabweni katika shule hiyo.
Mtwara. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa Mkoa wa Mtwara, (Takukuru) imezuia fedha zaidi ya Sh250 milioni zilizolipwa kinyemela kwa mzabuni kutoka katika akaunti ya shule ya Sekondari ya Mustapha Sabodo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Elisante Mashauri amesema kuwa fedha hizo zilitakiwa kujenga madarasa, mabweni na vyoo vya wanafunzi katika shule ya Sekondari Mustapha Sabodo.
Amesema kuwa baada ya kupokea taarifa za fedha hizo kulipwa kinyemela katika akaunti ya mzabuni walifanya uchunguzi Juni 6,2023 na kubaini kuwa kiasi cha Sh250 milioni kiliingizwa kwenye akaunti ya mazabuni Mubba General Supplies kutoka katika akaunti ya shule ya sekondari ya Mustapha sabodo bila uwepo wa nyaraka mbalimbali za idhini ya malipo hayo.
Aidha amesema kuwa malipo hayo hayakuwa na hati ya madai kutoka kwa mlipwaji kwakuwa hakuwahi kupeleka vifaa vya ujenzi wala kutakiwa kufanya hivyo licha ya kufanyika kwa malipo hayo.
Hata hivyo malipo hayo ni kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma sura ya 410 kama ilivyorejewa mwaka 2022 ambapo Takukuru ilifanya mahojiano na mlipwaji na kubainika kuwa hakuna kifaa chochote alichowahi kupeleka shuleni hapo.
“Inashangaza sana inawezekanaje mzabuni ambaye hajawahi kuomba zabuni shule hiyo alipwe pesa ambapo na yeye alikaa akisubuiria malekezo ya fedha hizo ambazo zilikuwa kwaajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa mabweni 3, madarasa 8 na matundu ya choo 13 yaliyokuwa yanajengwa shuleni hapo,” amesema Mashauri.
Baada ya mahojiano ya mlipwaji na Takukuru mkoa wa Mtwara ilimtaka mlipwaji kuzirejesha kwenye akaunti ya shule ili taratibu za manunuzi zifuatwe ambapo mlipwaji alitekeleza agizo hilo na kurejesha fedha hizo.