Takukuru yachunguza watumishi 11 wa Jiji la Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu utatuzi wa migogoro na kuwashughulikia watumishi wasio waadilifu.
Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inaendelea na uchunguzi wa watumishi 11 wa Jiji la Dodoma waliosimamishwa kazi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Oktoba 3, mwaka huu, Majaliwa aliwasimamisha kazi na kuagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Takukuru kuwafuatilia na kuwarejesha jijini Dodoma kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kupora maeneo ya wananchi na kugawa maeneo ya wazi.
Watumishi hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, Scorpion Philip, Lennis Ngole, Allen Mwakanjuki, Aisha Masanja, Augusta Primo, Azory William Byakanwa, Frezia Kazimoto, Premin Nzenga, Stella Komba na Thabiti Mbiyagi.
Akizungumza leo Oktoba 23, 2023, Silaa amesema watumishi hao wamekabidhiwa kwa Takukuru kwa mambo ambayo yana sura ya kijinai.
“Sisi kwetu tungependa kumalizana na mtu palepale sasa kama mtu ni wa onyo atapewa onyo, ndio sheria ya utumishi wauma inavyotaka. Sisi hatuwezi tunakuwa tunatuhumu wenyewe, tunaagiza wenyewe. Kama mtu anatakiwa kufukuzwa kazi sheria zitafuatwa,” amesema.
Aidha, Silaa amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo kuwaondoa watumishi wa kujitolea 25 ambao wanaonekana kuwa kero kwa watu wanaofika kupata huduma.
Amesema Aprili 25 mwaka huu wizara yake iliwaondoa kazini watumishi 106 wa kujitolea lakini bado kuna watumishi wa kujitolea 25 na kumuagiza mkurugenzi kuwaondoa.
Kuhusu madai ya viwanja, Silaa amesema tathimini ya awali iliyofanyika kwenye Jiji la Dodoma imebaini kuna madai viwanja mbadala 3,992 vinavyodaiwa kutokana na wananchi kupewa viwanja viwili (double allocation).
Amesema jiji limemaliza viwanja 1,102 ambavyo viko katika eneo la Nala, Lugala (1,035) na Mkonze (97) kwa ajili ya fidia na baadhi ya wananchi wameanza kupewa.
Amesema halmashauri hiyo inaendelea na upimaji wa viwanja 5,000 katika eneo la Mahomanyika ambavyo vitatumika kufidia wananchi wenye madai.
“Upimaji wa viwanja hivyo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 31 mwaka 2023. Nia yetu hadi kufikia Machi mwakani yale matatizo yote ambayo yaliyotokana na utendaji wetu kama Serikali yanafika mwisho,”amesema Silaa.
Kwa upande wa kliniki ya ardhi inayoendelea jijini Dodoma, Silaha amesema katika kipindi cha kati ya Oktoba 16 hadi 20 mwaka huu, jumla ya watu 3056 walihudumiwa.
Amesema hati miliki 1,474 zilitolewa papo hapo na maombi mapya 561 yalipokewa, waliopewa namba za kulipia 1,674 na migogoro ya ardhi 774 ilishughulikiwa.
“Utaratibu huu umekuwa ukitekelezwa nchi nzima nichukue nafasi hii kuwaelekeza makamishna wa ardhi wasaidizi wa mikoa yote kuendelea kuendesha kliniki hizo kwenye mikoa yao,”amesema.
Mmoja wa watu waliohudumia katika kliniki hiyo Dina Aseja amesema alipata changamoto kwa kiwanja chake alichogawiwa na jiji kiliuzwa kwa watu wengine na hivyo kusababisha mgogoro.
“Ombi langu kwa viongozi hawa kuwapatia hati wenzangu waliobakia ambao viwanja vyao viliuzwa kwa watu wengine na hivyo kuzua mgogoro wa ardhi,”amesema.