Tume huru yanukia, wadau waibana Serikali

Wadau wa demokrasia, Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, Viongozi wa Vyama vya Siasa, pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kwa ajili ya Mkutano Maalum wa Baraza hilo. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kuwasilisha bungeni miswada mitatu ya sheria za uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wadau wa demokrasia wameshauri iwekwe wazi kabla ya hatua hiyo kufikiwa, ili ijadiliwe kwa mizania ya ushirikishwaji.

Serikali imepanga kuwasilisha bungeni miswada hiyo ya sheria katika mkutano unaoanza Oktoba 31, mwaka huu.

Wadau hao pia mbali na miswada hiyo, wameitaka Serikali kuifanyia marekebisho madogo Katiba ya sasa ya mwaka 1977 ili iendane na mabadiliko ya sheria yanayokusudiwa.

Mbali na hayo, wametahadharisha changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa 2019 na 2020 zisirudiwe, wakieleza kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa mapema kwa kuangalia sheria, kanuni na taratibu zilizopo za kusimamia uchaguzi ili uwe huru, haki na amani.

Hayo yamejitokeza katika mkutano wa wadau zaidi ya 500 wa demokrasia ulioanza juzi, ukitarajiwa kuhitimishwa Septemba 13, 2023 jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, utafungwa leo na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.

Wadau walitoa hoja hizo juzi jioni baada ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratribu, Dk Jim Yonazi kuwasilisha taarifa ya jinsi Serikali ilivyotekeleza mapendekezo ya Kikosi Kazi cha wadau wa demokrasia.

Alifanya hivyo baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa Kikosi Kazi, Profesa Rwekeza Mukandala kuwasilisha mapendekezo ya kikosi hicho.

Katika taarifa hiyo ya Serikali, Dk Yonazi alisema miongoni mwa mapendekezo ya Kikosi Kazi ilikuwa kuruhusiwa mikutano ya hadhara, pendekezo ambalo Serikali imekwisha litekeleza.

Alisema pendekezo la mabadiliko ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uendeshaji na kupatikana wajumbe wa tume linafanyiwa kazi.

"Pendekezo hili limefanyiwa kazi na Serikali kupitia mapendekezo ya muswada mpya wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi ambao unakusudiwa kuwasilishwa na Serikali bungeni katika mkutano wa 13 wa Bunge utakaoanza Oktoba 31, 2023," alisema Dk Yonazi.

Alifafanua kuwa pendekezo la Tume hiyo kuwa na bajeti kwa wakati, hata baada ya kumalizika kwa uchaguzi, Dk Yonazi alisema nalo limefanyiwa kazi katika muswada huo.

Vilevile, alisema pendekezo kwamba Tume ya taifa Uchaguzi isilazimike kufuata amri au maagizo ya mtu au taasisi yoyote limezingatiwa.

Kuhusu pendekezo kwamba utendaji wa Tume ya Uchaguzi uhojiwe mahakamani, alisema linagusa hilo Katiba iliyopo ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 74(11) na kuwa litafanyiwa kazi kupitia utaratibu wa mchakato wa Katiba.

Dk Yonaz, pia alizungumzia pendekezo la kikosi kazi kuhusu marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, kuwa limefanyiwa kazi kupitia mapendekezo ya muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ambao pia unakusudiwa kuwasilishwa bungeni Oktoba mwaka huu.

Kikosi Kazi kilipendeza kulipatia Baraza la Vyama vya Siasa linaloundwa na vyama vyenyewe, mamlaka ya kushughulikia suala la uvunjifu wa maadili ya vyama vya siasa kupitia kamati yake ya maadili; na Msajili wa Vyama vya Siasa aandae mwongozo wa uchaguzi wa ndani ya vyama vya siasa.




Mapendekezo mengine

Kikosi Kazi pia kilipendekeza kuweka masharti ya idadi ya jinsi moja katika vyombo vya uamuzi wa vyama vya siasa isipungue asilimia 40 na kukitaka kila chama cha siasa kuwa na sera ya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli za chama husika.

Kuhusu kwamba ruzuku itolewe kwa vyama vyote tofauti na mfumo ulivyo sasa wa kuitoa kwa vyama vyenye wabunge na madiwani, Dk Yonazi alisema limefanyiwa kazi kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambao pia utakawasilishwa bungeni Oktoba.

Alisema kama ilivyoelezwa awali, lengo la kukidhi matakwa ya taratibu za utungwaji wa sheria, ni lazima kupata maoni ya wadau wengine ili kufanikisha tathmini ya kina, hivyo utekelezaji wa pendekezo hilo katika muswada wa sheria umezingatia maoni hayo.

“Baada ya muswada wa sheria kupitishiwa na Bunge na ukishasainiwa na Rais kuwa sheria ya nchi, baadhi ya masuala yatawekewa mkazo kupitia kanuni,” alisema.

Kuhusu bajeti ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa, Serikali imefanyia kazi na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ulionza Julai mwaka huu, Ofisi hiyo imeongezewa bajeti ya matumizi ya kawaida kutoka Sh2.51 bilioni mwaka jana hadi Sh5.02 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 99.5.


Wajumbe waja juu

Akichangia taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba alisema mabadiliko ya sheria zilizotajwa yanahitaji pia mabadiliko ya Katiba ili yaendane na mahitaji ya kikatiba na kisheria.

Profesa Lipumba alisema mapendekezo waliyotoa, likiwema la matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, mshindi wa urais kupatikana kwa zaidi ya asilimia 100, mgombea binafsi na uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi yanahitaji mabadiliko madogo ya Katiba.

“Napongeza Serikali kwa hatua ya kutaka kupeleka miswada bungeni, lakini tunaomba itupe ratiba ya utekelezaji ili kujua itakavyokuwa; uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ukafanyike kwa amani,” alisema Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti wa CUF.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo aliyesema wakati sheria hizo zikipelekwa bungeni; mabadiliko ya Katiba nayo yafanyike kwa pamoja.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliipongeza Serikali kwa kuyafanyia kazi mapendekezo ya kikosi kazi akisema, “hakuna ambako Serikali imesema haikubaliani na Kikosi Kazi, tumeona mikutano ya hadhara inaendelea.”

Kuhusu miswada kupelekwa bungeni, Jaji Warioba alisema, “sasa hapo ndiyo bado, kwa sababu hawajasema wamekubali yote yale ambayo Kikosi Kazi kimesema, kwa hiyo wakati wa kutafakari, tuombe Serikali itoe miswada hiyo ya kutosha ili iangaliwe na ikienda kwenye Bunge, mengi tutakuwa tumepiga hatua.”

Kutokana na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita, alisema alitarajia zingeanza kufanyiwa kazi na Serikali, hasa kisheria.

“Mwaka 2020, pamoja na mafanikio, kulikuwa na changamoto nyingi na kwa vyovyote vile, hata kama isingekuwa sasa, mimi nilitegemea angalau ndani ya Serikali, changamoto zile zilionekana na hatua zingechukuliwa ama kisheria au kikanuni au utaratibu wa kuepusha zisije zikatokea mwaka 2024 na 2025.

“Wote tunajua kilichotokea mwaka 2019 na 2020, ilikuwa mara ya kwanza, Watanzania wamezoea kupiga kura, huwa zinatokea changamoto lakini si kama ilivyokuwa mwaka 2020, ilikuwa mara ya kwanza kwa wagombea wengi kuenguliwa kwenye uchaguzi, tuliona matumizi makubwa ya fedha katika kila hatua kuanzia kwenye uteuzi hadi kampeni,” alisema.

Jaji Warioba alisisitiza kama wanataka kuepusha hayo, waanze kujiandaa kwa kuangalia sheria, kanuni na hasa taratibu za kusimamia uchaguzi ili wasipate matatizo kwenye uchaguzi ujao.


Vifungu vya kubadilishwa



Askofu wa Kanisa la Moravian Uamsho, Emmaus Mwamakula alipendekeza mabadiliko ya sheria yaende sambamba na mabadiliko ya vifungu vya Katiba.

Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Askofu Mwamakula ni pamoja na vifungu vya Katiba vya 39 (2), 41(6,7), 42, 66(a, b), 67, 71 74(2,6), 75(1,2,3,5,6), 76 na 77. Pia, alipendekeza kuongezwa kifungu kitakachoruhusu matokeo ya uchaguzi kuhojiwa mahakamani.

“Maboresho ya sheria yakifanyika lakini tukaacha vifungu vyenye nguvu kwenye Katiba yetu, tutakuwa hatujafanya jambo la maana,” alisema Askofu Mwamakula.

Mwanadiplomasia, Balozi Amina Salum Ali, pia aliitaka Serikali kuiweka wazi miswada hiyo ili wadau waichambue kabla ya kupelekwa bungeni.

“Bado kuna watu watakuwa na hofu kama tulivyotoa hofu kwa mara ya kwanza, hizi sheria zinazokwenda bungeni Oktoba na sasa tupo kipindi cha Septemba na katika dhana ileile shirikishi, tunapaswa kuzijua, maoni yafanyike ili wabunge wapate mapendekezo mazuri na kujua nini kinakwenda kufanyika,” alisema Balozi Ali ambaye mwaka 2015 aliomba kuteuliwa kugombea urais ndani ya CCM na akashika nafasi ya pili baada ya Hayati John Magufuli.

Waziri mkuu mstaafu, Mizengo Pinda naye alikuwa miongoni mwa walioitaka Serikali kuiweka wazi miswada hiyo ili wadau wakiwamo walioshiriki mkutano wa demokrasia wakaichambua vilivyo.

“Mimi naomba sana, wadau wakubwa wa ajenda hii ni hawa tuliopo hapa, Bunge lina utaratibu mzuri sana wanapokuwa wanapeleka miswada, kabla ya kufika hatua mbalimbali kunakuwa na hatua ya kukutana na wadau kuwashirikisha ili kupata mawazo ya kutosha.

“Ningeomba Bunge likaombwa kukutana na hawa wadau, si lazima wote, ila baadhi ili kukutana na kamati husika, naona kushirikishana kwa wadau hawa ni muhimu sana,” alisema Pinda ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Pinda aligusia suala la rushwa nyakati za uchaguzi akisema hatua hiyo inaweza, “kutupeleka kubaya,” na akashauri sheria ya Takukuru iangaliwe vizuri ili kudhibiti rushwa na kupata viongozi wanaopatikana bila rushwa.

Akizungumzia suala la maoni kuhusu muswada, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya utawala, katiba na sheria, Joseph Mhagama alisema wana njia mbili za kupokea maoni wanapoijadili miswada. Mosi, kuwaita wadau kufika mbele ya kamati au kuyawasilisha kwa njia ya maandishi.

Alisema miswada hiyo ambayo Serikali imesema itawasilishwa Oktoba, itasomwa kwa mara ya kwanza na kujadiliwa katika mkutano unaofuata wa Februari mwakani. “Na unaweza kuja kwa njia ya hati ya dharura kwa kibali maalumu cha Rais,” alisema.

Hata hivyo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alitofautiana na Mhagama juu ya miswada ya hati ya dharura.

“Hili tusiliruhusu, tuipeleke kwa utaratibu wa kawaida, historia inaonyesha miswada iliyokwenda kwa hati ya dharura imezalisha sheria zisizo nzuri,” alisema.


Ofisi ya msajili

Alipopata fursa ya kuchangia, Msajili wa zamani wa vyama vya siasa, John Tendwa alisema kuna haja ya kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ili ipanuke na kuwafikia wananchi, ili iweze kusaidia katika utoaji wa elimu kwa wapigakura kwa kushirikiana na wadau wengine.

Alipendekeza kwamba elimu ya mpigakura itolewe na ofisi hiyo, jambo ambalo litasaidia katika ulinzi wa amani kwa kuwashirikisha wananchi na kuongeza idadi ya wanaokwenda kupiga kura, baadaye itakuwa ni sehemu ya maadili ya Watanzania katika demokrasia yao.

“Wakati wangu nilianzisha kanda saba, sijui zilikufaje. Kama Ofisi ya Msajili itakuwa katika kanda, itasaidia kushirikiana na wadau kutoa elimu, hiyo itaongeza idadi ya wanaokwenda kupigakura, amani itakuwepo na itakuwa ni sehemu ya maadili yetu,” alisema Tendwa.

Tendwa alipendekeza pia vyama vidogo navyo vipate ruzuku kwa ajili ya uchaguzi ili kuviwezesha kufika kwa wananchi kunadi sera zao na kuwapa nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Tufanye utaratibu ambao utaviwezesha vyama vichanga kupata election funds (fedha za uchaguzi) kwa ajili ya kampeni za uchaguzi. Uholanzi wanafanya hivyo, sisi pia tuna TCD ambayo inaweza kuratibu mfuko huu,” alisema Tendwa.


Kujidanganya wenyewe


Katika mjadala huo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza aliunga mkono mabadiliko ya sheria ili kufanya chaguzi zijazo kufanyika kwa uhuru na amani.

“Kwenda kwenye uchaguzi ujao bila kufanyika marekebisho yoyote tutakuwa tunajidanganya wenyewe,” alisema.

Askofu Bagonza alisema marais waliopita walifanya mambo mengi, akisisitiza kwamba Rais Samia anatakiwa kuwafanyia Watanzania jambo moja la kujenga mfumo mzuri wa demokrasia nchini.

“Akituwekea mfumo mzuri wa kidemokrasia, hatutamsahau maisha yetu yote,” alisema Askofu Bagonza.


CCM yajibu mapigo

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Anamringi Macha alijibu hoja ya mjumbe mmoja wa mkutano huo aliyehoji kwa nini chama hicho hakichoki kuitawala nchi hii, licha ya kufanya makosa mengi yaliyolifikisha Taifa hapa lilipo na kufikiria kuachia ngazi ili wengine watawale.

“Katiba ya CCM inasema nia yetu ni kushinda uchaguzi na kukamata madaraka na hakuna katiba ya chama chochote inayosema kwamba wao watashiriki tu uchaguzi na kuishia hapo,” alisema Macha.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wasira alisema amani katika nchi hii ina historia yake na kwamba inaweza ikawepo au ikatoweka na wananchi ndiyo wana wajibu wa kulinda amani hiyo.

Alipingana na maoni ya washiriki wengine waliopendekeza kujengwa kwa Taasisi za kidemokrasia, akisema hata nchi zenye taasisi hizo zimekuwa na changamoto za amani kila baada ya uchaguzi.

“Amani italetwa na kauli zetu, kama zinaashiria uvunjifu wa amani, hatutakuwa na amani. Sisi ni binadamu, tujenge utamaduni wa kuwa na kauli ambazo haziwagawi watu. Tutoe kauli ambazo tutashindana bila kupigana,” alisema Wasira.


Polisi lawamani, Sagini ajibu

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagidi alijibu lamawa mbalimbali zilizoelekezwa kwa Jeshi la Polisi kuhusu kushiriki kuvuruga uchaguzi pamoja na Wizara ya Tamisemi kutoshiriki kusimamia chaguzi za serikali za mitaa.

“Jeshi la Polisi tunalilaumu kwa sababu lipo, lakini lina jukumu la kulinda usalama wa wananchi na mali zao, kila siku inayokwenda kwa Mungu, ni dhamana waliyopewa hawa watu. Tunaweza kuwalaumu kwa uchache wao au dhamana waliyopewa lakini wanafanya kazi kubwa,” alisema Sagini.

“Siku moja niliwahi kusema tulitoe hili Jeshi la Polisi huko kwa wananchi sijui hali itakuwaje, tunalilaumu kwa sababu lipo.”

Alitolea mfano siku moja wananchi “walikuwa wanasema polisi ni wengi barabarani, wakaamua kujipunguza kwenye barabara ya Tegeta (Dar es Salaam), Ijumaa moja hivi watu walifika majumbani kwao saa 6 usiku kwa sababu hatutaki kutii sheria.”

“Kuna lugha zinatolewa dhidi ya Jeshi la Polisi kwa haohao ambao wanapaswa kukulinda, unawazodoazodoa, hazifai. Lakini mwelekeo wa Rais Samia hasa zile 4R, umebadili utendaji wa Jeshi la Polisi na mimi nitaendelea kusikiliza maoni ya wadau na tutakwenda kuyatumia mawazo ya wadau,” alisema.

Sagini aliyewahi kuwa Katibu Mkuu-Tamisemi alisema kuna vijiji na mitaa waliyoshinda wapinzani, “na kutangazwa kuwa wenyeviti wa mitaa” kwa hiyo kama kuna hoja, tuzijadili na kuona jinsi ya kufanya lakini kwa vyama viandae wagombea wazuri.

Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu hoja iliyoibuliwa na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo, Abdul Nondo aliyesema kama marekebisho yoyote ya sheria za uchaguzi yasipofanyika kabla ya uchaguzi kinyume chake ni kwenda kuvuruga amani.

"Katibu mkuu, jana (juzi) katika wasilisho lake hakusema lolote kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, Tamisemi haipaswi kusimamia uchaguzi, unapaswa kusimamiwa na tume ya uchaguzi," alisema Nondo.

"Uchaguzi huu kwenda kusimamiwa na Tamisemi chini ya Waziri anayeteuliwa na Rais hauwezi kuwa huru na haki na yaliyojitokeza huko nyuma yatajirudia.

“Sisi mapendekezo yetu ni uchaguzi huu usimamiwe na Tume ya uchaguzi na hii iwemo kwenye sheria hizi ambazo tumeambiwa zitapelekwa katika Bunge la Oktoba na Novemba," alisema.