Watumishi wa mahakama kortini kwa makosa 14

Muktasari:

  • Washitakiwa hao watatu ambao ni watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara sasa wana jumla ya kesi tatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara za Uhujumu uchumi wa zaidi ya Sh132 milioni.

Mtwara. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) mkoani hapa leo imewapandisha tena kizimbani wahasibu wawili na mtunza kumbukumbu wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, kwa kesi ya uhujumu uchumi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Charles Mnzava washitakiwa hao Beda Nyasira, (47), Theodosia Mtelani (37), wote wahasibu, pamoja na mtunza kumbukumbu, Mahafudhi Chinenda (42), wameshitakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi namba 6 ya mwaka 2023 yenye jumla ya makosa 14.

Mwanasheria wa Takukuru Mtwara, Naftal Mnzava amesema kuwa washitakiwa hao kwa pamoja walitenda shitaka hilo la uhujumu uchumi wa Sh56.2 milioni kati ya Juni 2020 na Mei 2022 kutoka katika akaunti maalum ya wanufaika wa mirathi iliyopo Benki kuu ya Tanzania, (BoT).

Naftali ameieleza Mahakama hiyo kuwa katika kosa la kwanza, watu hao kwa pamoja wanashitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka kwa kuifanyia fujo sheria na kumlipa kiasi cha zaidi ya Sh56 milioni Said Bakari Mitindo, huku wakiwa watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara na wakijua wanaemlipa sio mnufaika wa mirathi wala hana kesi yoyote mahakamani hapo.

Kosa la pili hadi la kumi na mbili ni la kuitia mamlaka hasara kwa kipindi tofauti kwa kumlipa posho, hela ya chakula na malipo mengine Said Bakari Mitindo huku wakijua sio mnufaika wa kesi ya mirathi.

Katika kosa la kumi na tatu wameshtakiwa kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwenye akaunti ya maalum ya mirathi huku kosa la mwisho likiwa ni utakatishaji fedha kinyume cha sheria.

Fedha hizo zimelipwa katika akaunti mbili za benki za CDRB na NMB zinazomilikiwa na Said Bakari Mitindo.

Washitakiwa wote wamekana makosa yao 14 na wamerudishwa rumande hadi Oktoba 18, 2023 watakapoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Washitakiwa hao wanatetewa na Wakili Radhia Luhuna.

Washitakiwa hao pia wana kesi mbili za Uhujumu uchumi namba 4 na 5 za mwaka huu ambazo kwa pamoja ni zaidi ya Sh132.