Takukuru yapewa rungu wabadhirifu MSD

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwashughulikia watumishi wote watakaoonekana wamehusika katika ubadhirifu wa manunuzi na fedha katika Bohari ya Dawa (MSD).

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwashughulikia watumishi wote watakaoonekana wamehusika katika ubadhirifu wa manunuzi na fedha katika Bohari ya Dawa (MSD).

Takukuru ambao wameweka kambi katika taasisi hiyo kwa sasa, watafanya ukaguzi katika yale yaliyoonekana katika ripoti ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere pamoja na maeneo mengine ikiwemo fedha za Uviko-19.

Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 9, 2022 alipofanya ziara MSD kwa lengo la kufanya ukaguzi kutokana na baadhi ya watendaji kutuhumiwa kukiuka kanuni za manunuzi ya umma kama alivyoahidi siku tano zilizopita akiwa Arusha.

“Takukuru wapo hapa, mimi siwezi kusema chochote nimekuja kutoa maelekezo nini kifanyike. Yeyote aliyehusika kwenye ubadhirifu achukuliwe hatua ili utendaji mpya uanze kazi paliwa pasafi na MSD irudi katika nafasi yake na nimeshatoa maelekezo kwa Waziri wa Afya,” amesema.

Akitaja ubadhirifu uliofanyika, Majaliwa amesema watumishi watatu ambao walikwenda kufanya manunuzi nchini China na kutumia kiasi cha Sh216 milioni kama posho wataingia matatani kwakuwa walifanya kazi ambayo ingeweza kufanywa na Balozi wa Tanzania nchini China.

“Hakuna document yoyote halali inayoonyesha na mlifanya manunuzi huko bila zabuni, wala bodi haikulipitisha hilo hii inaonyesha lilikuwa wazo la mtu mmoja?” Amehoji Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Afya kuunda haraka bodi ya kuwarugenzi ili mwenyekiti wake aanze kazi mara moja.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema tayari mchakato wa kufanya mabadiliko katika ngazi zote za utendaji, “Tumeshaanza mchakato wa kufanya mabadiliko na maagizo yote tumeyapokea na tutayafanyia kazi.”