Tamisemi kutolea mwongozo matamko ya Makonda, Mnyeti

Muktasari:

  • Jumatatu iliyopita, Makonda ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa tamko la kusimamisha mabaraza hayo katika mkoa wake kabla ya Mnyeti wa Mkoa wa Manyara kutamka kuvunja baraza la Ardhi Kata ya Murray, wilayani Mbulu juzi.

Hatua ya wakuu wawili wa mikoa, Paul Makonda na Alexander Mnyeti kutoa matamko ya kusimamisha shughuli au kuvunja mabaraza ya kata, Serikali imesema inaandaa mwongozo kuhusu suala hilo.

Jumatatu iliyopita, Makonda ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa tamko la kusimamisha mabaraza hayo katika mkoa wake kabla ya Mnyeti wa Mkoa wa Manyara kutamka kuvunja baraza la Ardhi Kata ya Murray, wilayani Mbulu juzi.

Alipotafutwa jana kuzungumzia hatua za wakuu hao, katibu mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mussa Iyombe alisema, “Tunakamilisha mwongozo kuhusu suala hilo wiki hii, fanyeni subira.”

Uamuzi wa Mnyeti

Mnyeti alitangaza uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kunyanyaswa, kuombwa rushwa na kunyimwa haki.

Akizungumza katika kata hiyo alisema hawezi kuliacha baraza hilo liendelee kufanya kazi ilihali wananchi wanalalamika kukosa haki.

Alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Anna Mbogo kuanza mchakato wa kupatikana viongozi wapya waadilifu wa baraza hilo la kata ili waendelee kuwatumikia wananchi na kuagiza mikutano ya wananchi kuwachagua wajumbe wengine ianze upya.

“Tafuteni watu waadilifu, wenye weledi na hofu ya Mungu, ambao wanaweza kuwahudumia wananchi ili washike nafasi hizo na kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alisema Mnyeti.

Hatua ya Mnyeti ilitokana na malalamiko kutoka kwa mkazi wa Murray, Michael Amme kwamba baraza hilo halitendi haki na wananchi wanyonge wanaonewa. Amme alidai kwamba familia yake iliporwa eneo kutokana na uamuzi wa baraza hilo.

Mjumbe wa baraza hilo, Verani Anthony alisema wananchi wanapaswa kupatiwa elimu kuhusu utendaji kazi wa baraza hilo kwa kuwa wao hutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Kuhusu Makonda

Juzi, Iyombe akizungumza na mwandishi wetu kuhusu tamko la Makonda, alisema mkuu huyo wa mkoa ameshatoa ufafanuzi kwa maandishi akikana kusimamisha mabaraza hayo kufanya kazi.

“Tulimtaka atuandikie barua ya kutueleza na tayari ameshafanya hivyo, tumemalizana naye kwa maandishi, hakusimamisha mabaraza hayo kufanya kazi,” alisema Iyombe.

Hata hivyo, katibu mkuu huyo alipoulizwa kama Makonda alitakiwa kuandika barua baada ya kuvunja kipengele kipi cha sheria kutokana na tamko lake, alisema:

“Sitaki kusema alivunja kipengele ni wewe wasema, ninachosema kama kiongozi lazima unachokisema wananchi wakielewe, kulikuwa na maswali watu wanahoji kuhusu suala hilo ndiyo maana tukamtaka atufafanulie na amefanya hivyo kwa maandishi. ”

LHRC wampinga Makonda

Kauli ya Makonda kuhusu Mahakama imepingwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kikimesema imeingilia muhimili huo wa dola.

Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Felista Mauya alisema jana kuwa katika mkutano uliofanyika Februari 10 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Makonda alikaririwa akitamka kuwa, “Mahakama haitaki kuguswa kwa kisingizio cha muhimili mwingine, wamechukua nafasi ya Mungu na mimi ni mteule wa Mungu lazima niwaseme.”

Mauya alisema, “Huku ni kushambulia utendaji wa Mahakama kinyume cha Katiba aliyoapa kuilinda.”

Alisema Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki Tanzania itakuwa Mahakama.

“Wakati huohuo Ibara ya 107B inasisitiza uhuru wa Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake, kwa hiyo kwa mujibu wa ibara hii mihimili mingine ya dola na watendaji wake hawapaswi kwa namna yoyote ile kuingilia utendaji wa Mahakama,” alisema.

Alisema kituo hicho kinawakumbusha viongozi wa Serikali na wanasiasa kuwa hawana mamlaka kisheria kuingilia utendaji kazi chombo hicho wala kuelekeza utendaji badala yake wanapaswa kuheshimu na kufuata utaratibu katika upatikanaji wa haki.

Kuhusu mabaraza ya ardhi, Mauya alisema sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi inamtaja waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi kuwa na mamlaka juu ya mabaraza ya ardhi ya kata.

“Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi namba 216, Mwaka 2002 kinayatambua mabaraza ya kata kama Mahakama ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa ngazi ya kata, hivyo kwa mujibu wa sheria hizi wakuu wa mikoa hawana mamlaka ya kusimamisha kuendesha wala kuelekeza utendaji,” alisema.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga alisema lengo la tamko hilo ni kutaka umma ufahamu kuwa kitendo cha wakuu wa mikoa kuingilia Mahakama si sahihi.

“Kwanza wajue ni utaratibu upi uliopo kisheria kwa kuwa kuna Mahakama kitengo cha ardhi, mabaraza ya kata lakini tukisema tuwakusanye kila mmoja aeleze shida yake tutakuwa tunatatua kero bila sheria,” alisema.

Waraka wa Tume

Andiko la Tume ya Kurekebisha Sheria kwenye mapitio ya mfumo wa utoaji haki katika mashauri ya madai, sehemu ya III la Julai 2012 linalopatikana kwenye mtandao linaelezea utekelezaji wa Sheria ya Mabaraza ya Kata ya mwaka 1985.

Linasema mabaraza hayo yanapaswa kuwa chini ya usimamizi wa Serikali za Mitaa na wajumbe huteuliwa na kamati ya maendeleo ya kata. Baraza huongozwa na mwenyekiti anayeteuliwa na halmashauri husika.

Majukumu ya baraza ni kutunza amani kwenye kata, kutatua migogoro, kusuluhisha ndoa na kusimamia utekelezaji wa sheria ndogondogo kama zilivyopitishwa na halmashauri husika.

Baraza pia lina uwezo wa kutatua migogoro yote ya ardhi katika kata, iwe ardhi iliyopimwa au isiyopimwa.

Uteuzi wa viongozi wa mabaraza

Kwa mujibu wa sheria, uteuzi wa mwenyekiti wa baraza la ardhi na nyumba la wilaya unafanywa na wizara inayohusika na masuala ya ardhi wakati uteuzi wa wajumbe wa baraza la kata unafanywa na halmashauri husika.

Hata hivyo, katika andiko hilo, Tume ilibaini kuwa vyombo vilivyopewa uwezo wa kuajiri au kufanya uteuzi wa nafasi hizo vina mwingiliano wa kisiasa ambao unaweza kuingilia utendaji kazi wa maofisa wanaowateua au kuwashawishi katika uamuzi wanaoyafanya.

Imeandikwa na Kalunde Jamal, Joseph Lyimo, Asna Kaniki na Allence Juma