Tanapa yafufua ujenzi hoteli ya kitalii Chato

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Said Nkumba (wa tatu kushoto) akiwaongoza viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na waandishi wa habari kutembelea mradi wa ujenzi wa Hoteli ya nyota tatu inayojengwa Kijiji cha Rubambagwe wilayani humo. Picha na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) linajenga Hoteli ya Kitalii ya nyota tano wilayani Chato, mkoani Geita, yenye lengo la kuvutia watalii katika hifadhi za mwambao huo zikiwemo za Burigi-Chato na ile ya Kisiwa cha Rubondo.

Chato. Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya nyota tatu katika Kijiji cha Rubambagwe, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita uliokuwa umesimama kutokana na ukosefu wa fedha, unatarajia kuendelea baada ya Serikali kutoa Sh480 milioni.

Hoteli hiyo inajengwa na Suma JKT ikiwa na lengo la kuchochea utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo na Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato.


Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la mradi hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Said Nkumba alisema tayari fedha hizo zimeingia kuendelea ujenzi huo, ikiwa ni ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa kwenye mazishi ya Rais wa tano, Hayati John Magufuli kuwa angeendeleza miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake ikiwemo Hoteli hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Nkumba amesema miradi kama Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la la JPM maarufu daraja la Busisi  na mingine imeendelea kutekelezwa kwa ufanisi.

Nkumba amesema miongoni mwa miradi hiyo inayoendelezwa imo ya wilayani Chato ambayo ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda na Hoteli hiyo ya kitalii inayotarajiwa kukamilika Desemba 2024.

“Ahadi anakwenda kuendeleza miradi iliyoachwa na mtangulizi wake ameendelea nayo na hapa kulikuwa na tatizo la kuendelea na mradi huu wa hoteli. Tulikwisha kupokea Sh700 milioni na tayari Sh480 milioni zimeingia ili kuuendeleza.

“Jitihaza za Serikali zinajidhihirisha kuwa tunaikuza sekta ya utalii na kufanya utalii kwa maeneo mbalimbali kwenye Hifadhi ya Burigi-Chato na Rubondo. Hapa kutakuwa na kila kitu kinachojitosheleza na mradi huu tunausimamia vizuri kuhakikisha unakamilika kwa wakati.”

Mkuu huyo wa wilaya amesema hadi kukamilikwa kwake, mradi huo unatarajia kugharimu takribani Sh11 bilioni na wao kwa niaba ya wilaya watahakikisha wanausimamia kikamilifu.

“Lakini mradi huu ni kichochea tu, kuna miradi mingine ya kitalii na watalii wanatembelea hifadhi zetu lakini wakifika hapa wanakosa maeneo ya kulala, sasa wataweza kulala hapahapa na kuchochea maendeleo ya maeneo haya,” alisema.

Mhandisi wa Jengo kutoka Suma JKT, Abdul Kobeza amesema wanajenga hoteli ya hadhi ya nyota tatu itakayokuwa na vyumba 30 kati yake kumi vya kawaida na 20 vya hadhi ya juu vikiwa na kila kitu ndani.

Amesema kutakuwa na kumbi za mikutano nne na kati yake tatu zinaweza kukodishwa kwa watu mbalimbali.

Kobeza amesema kutakuwa na mighahawa na kutajengwa viwanja vya mipira na mabwawa ya kuogelea pamoja na nyumba za watu mashuhuli, akiwemo Rais iwapo atambelea eneo hilo na kuhitaji kulala, ili kuifanya kwenda na hadhi ya nyota tatu.

Amesema kutoka hotelini hapo kwenda Kisiwa cha Rubondo si mbali ni takribani kilomita 20 na kupita majini ni karibu zaidi.

Mhandisi huyo amesema kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 67 na wanatarajia kukamilika Desemba mwaka huu.


Alichobaini CAG

Mwaka jana hoteli hiyo ilitajwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 kuwa kulikuwa na upungufu katika utekelezaji wa ujenzi wake.

CAG Charles Kichere alisema ukaguzi huo wa taratibu za ununuzi na usahihi wa malipo yanayofikia Sh12.9 bilioni ulibaini kabla ya kuanza kwa mradi huo, Tanapa ilifanya malipo ya awali ya Sh500 milioni kwa Suma-JKT Agosti 2, 2019 na baadaye Februari 17, 2020 ilifanya malipo mengine ya Sh500 milioni, hivyo kufanya jumla kuwa Sh1 bilioni,” alisema CAG Kichere.

CAG alisema Tanapa ilianza mchakato wa ununuzi Julai 11, 2019 kupitia fomu ya ununuzi Na. 2, lakini bodi ya zabuni ilibadilisha njia ya ununuzi kutoka zabuni ya kitaifa ya ushindani na kuwa njia isiyo ya ushindani kwa mzabuni mmoja.

CAG huyo alisema, tathmini ya mkandarasi ilionyesha Kampuni ya Suma-JKT ilikuwa na uzoefu wa chini ya miaka mitano na haikuwa na wastani wa mauzo ya ujenzi wa Sh1 bilioni kila mwaka, kama ilivyotakiwa kwenye maelekezo kwa wazabuni.

“Pamoja na upungufu huo, Machi 26, 2020, baraza la wadhamini la Hifadhi za Taifa Tanzania iliingia mkataba na. PA/037/2019-20/W/HQ/139 wenye thamani ya Sh11 bilioni na Kampuni ya Suma-JKT kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa miezi 12 kuanzia Aprili 14, 2020,” alisema

Alisema ripoti ya utekelezaji wa mradi ulionesha hadi Oktoba 31, 2021, Hifadhi za Taifa Tanzania ilikuwa imelipa Sh4.1 bilioni (asilimia 37 ya gharama za mradi) na utekelezaji wa asilimia 40 bila kuendelea na ilibaki vilevile hadi wakati wa ukaguzi huo Desemba 20, 2021.

Kutokana na upungufu huo, CAG Kichere alisema, “ninapendekeza Hifadhi za Taifa Tanzania izingatie sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma wakati wa utekelezaji wa miradi ya baadaye.”


Wenyeji wachekelea

Mkazi wa eneo hilo, Katarina Charles alisema kukamilika kwa hoteli hiyo itakuwa ni fursa za kuchochea maendeleo yao binafasi na wilaya.

“Yaani sisi kama majirani wa eneo hili tutaneemeka kwa vitu vingi, tutapokea wageni wa kila aina na maendeleo tutayatapa kwani tutatengeneza vitu vya kuwavutia watalii. Hata kuuza miwa na karanga.”

Naye Mariam Rusangija alisema kukamilika kwa ujenzi huo wananchi wanaweza kupata ajira na kufanya biashara: “Najua ujenzi ukikamilika hatuwezi kukosa hata ajira. Unajua mpaka sasa hakuna hoteli kama hii na hii itakuwa ya kwanza, hivyo tunasubiri tu ikamilike.”

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Dk Immani Kikoti amesema tangu Rais Samia alipozindua filamu ya Royal Tour kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watalii wa kutoka nje na ndani kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

Dk Kikoti amesema mikoa ya kaskazini imejipanga vizuri kwa kuwa na hoteli nyingi, tofauti na maeneo mengine ikiwemo hifadhi hizo za Burigi- Chato, Rubondo na hifadhi zingine ambazo ziko mkoani Kagera zinazohitaji kuwa na maeneo mazuri ya kufikia wageni.

“Eneo hili ni maarufu sana kwa ajili ya utalii, jinsi utalii unavyopanuka na Serikali kutangaza vivutio kutakuwa na wageni wengi wanaohitaji kupata sehemu nzuri za kufikia,” amesema