CAG abaini udhaifu ujenzi wa hoteli Chato

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Charles Kichere wakati akisoma ripoti yake mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma Alhamisi, Aprili 6, 2023. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Mdhibiti Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebainisha upungufu wa utekelezaji wa mkataba wa ujenzi wa Hoteli ya nyota tatu eneo la Rubambangwe-Chato, mkoani Geita.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imebaini upungufu katika maeneo kadhaa wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Hoteli ya nyota tatu eneo la Rubambangwe-Chato, mkoani Geita.

 Ripoti hiyo ya CAG Charles Kichere aliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma, jana Alhamisi, Aprili 6, 2023 alisema, alifanya ukaguzi maalum wa Hifadhi ya Taifa Tanzania wa  mapitio ya taratibu za ununuzi na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hoteli hiyo pamoja na usahihi wa malipo yanayofikia Sh12.9 bilioni zilizotolewa na Hifadhi za Taifa Tanzania.

CAG alisema ukaguzi huo umebaini maeneo kadhaa yenye upungufu akisema Julai 5, 2019, Hifadhi za Taifa Tanzania ilisaini mkataba wa makubaliano na Kampuni ya Suma JKT kwa ajili ya ujenzi wa hoteli hiyo eneo la Rubambagwe-Chato, ili mkandarasi akabidhiwe eneo la mradi kabla ya mkataba kusainiwa.

“MoU ilibainisha makadirio ya gharama za mradi wa Sh1 bilioni kwa kuwa gharama halisi za mradi hazikuanzishwa wakati huo.

Kabla ya kuanza kwa mradi huo Oktoba 28, 2019, Tanapa ilifanya malipo ya awali ya Sh500 milioni kwa Suma-JKT Agosti 2, 2019 na baadaye Februari 17, 2020 ilifanya malipo mengine ya Sh500 milioni, hivyo kufanya jumla kuwa Sh1 bilioni,” alisema CAG Kichere

Alisema Hifadhi za Taifa Tanzania ilianza mchakato wa ununuzi Julai 11, 2019 kupitia fomu ya ununuzi Na. 2, ambapo bodi ya zabuni ilibadilisha njia ya ununuzi kutoka zabuni ya kitaifa ya ushindani na kuwa njia isiyo ya ushindani kwa mzabuni mmoja.

CAG huyo alisema, tathmini ya mkandarasi ilionesha Kampuni ya Suma-JKT ilikuwa na uzoefu wa chini ya miaka mitano na haikuwa na wastani wa mauzo ya ujenzi wa Sh1 bilioni kila mwaka kama ilivyotakiwa kwenye maelekezo kwa wazabuni.

“Pamoja na upungufu huo, Machi 26, 2020, baraza la wadhamini la Hifadhi za Taifa Tanzania iliingia mkataba na. PA/037/2019-20/W/HQ/139 wenye thamani ya Sh11 bilioni na Kampuni ya Suma-JKT kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa miezi 12 kuanzia Aprili 14, 2020,” alisema

Alisema ripoti ya utekelezaji wa mradi ilionesha hadi kufikia Oktoba 31, 2021, Hifadhi za Taifa Tanzania ilikuwa imelipa Sh4.1 bilioni (asilimia 37 ya gharama za mradi) na utekelezaji wa asilimia 40, bila kuendelea ilibaki vilevile hadi wakati wa ukaguzi huu Desemba 20, 2021.

Kutokana na upungufu huo, CAG Kichere alisema, “ninapendekeza Hifadhi za Taifa Tanzania izingatie sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma wakati wa utekelezaji wa miradi ya baadaye.”