Tanesco yasitisha kuzima mfumo wa ununuzi Luku

Muktasari:
- Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imetangaza kusitisha matengenezo ya mfumo wa manunuzi ya luku ambao ungesababisha wateja washindwe kununua umeme kwa siku nne kuanzia saa 4 usiku hadi saa 1 asubuhi.
Dar es Salaam. Saa chache baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza matengenezo kwenye kanzidata ya mfumo wa luku ambayo yangesababisha kukosekana kwa huduma hiyo, matengenezo hayo yamesitishwa.
Taarifa iliyotolewa asubuhi ya leo Jumatano na Meneja Mwandamizi wa Tehama wa shirika hilo, Cliff Maregeli alisema matengenezo hayo ya siku nne yalikuwa yaanze Agosti 22 - 25, 2022 kuanzia saa 4 usiku hadi saa 1 asubuhi.
Alisema kutokana na matengenezo hayo, wananchi wasingeweza kununua umeme kwa njia ya Luku.
Hata hivyo, haijachukua muda kupita ambapo Tanesco imetolewa taarifa nyingine iliyoeleza kusitishwa kwa matengenezo hayo hadi pale watakapotoa taarifa ya kuanza kwa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Maregeli, alisema lengo la matengenezo hayo ni kuongeza ufanisi katika mfumo wa Luku.
"Matengenezo haya muhimu yanalenga kuongeza ufanisi katika mfumo wa Luku ili kuwahudumia wateja wetu kwa ufanisi zaidi," alisema Maregeli.