Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanganyika Schools yatozwa faini Sh5 milioni

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania(Tira), Baghayo Saqware akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Baghayo Saqware amesema kwa muda wote mlalamikaji aliamini shule imesajiliwa kutoa huduma za bima na ina mpango mzuri wa huduma za bima kwa watoto wake wanapokuwa shuleni hadi siku mtoto wake (jina linahifadhiwa), aliporudi nyumbani akiwa amevunjika mguu bila kupatiwa huduma yoyote ya kimatibabu.

Arusha. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) imetoza faini ya Sh5 milioni Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya Tanganyika kutokana na kukusanya ada za bima kwa muda wa miaka 10 bila kusajiliwa kinyume na kifungu cha 161(1) cha Sheria ya Bima sura ya 394.

Aidha shule hiyo imetakiwa kurudisha fedha za bima za afya kwa muda wa miaka tisa iliyokusanywa kutoka kwa Alexander Oyage, alizokuwa analipa kwa watoto wake wawili kwa kipindi hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo, Kamishna wa Mamlaka hiyo nchini, Baghayo Saqware amesema Tanganyika Schools hutoza ada ya bima kila mwaka Sh200,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi na Sekondari na Sh 90,000 kwa shule ya awali.

Amesema kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 2014 hadi mwaka 2023, shule imekusanya zaidi ya  Sh207.6 milioni, fedha walizotumia kununua seti ya huduma ya kwanza na kuwahudumia kimatibabu wanafunzi wanaopatwa na majanga ya kuumwa wanapokuwa shule kuanzia wanapoanza masomo hadi jioni wanapomaliza.

Juhudi za kupata uongozi wa shule hiyo kuzungumzia suala hilo zilikwama baada ya waandishi waliofika shuleni hapo kuelezwa kuwa mkurugenzi wa shule hiyo hayupo Arusha kwa sasa na waliopo hawana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo hadi atakaporejea na kuzungumza mwenyewe.

Hata hivyo, kamishna huyo amesema Januari 16,2023 mamlaka hiyo kupitia ofisi za kanda ya Kaskazini ilipokea malalamiko ya mzazi huyo aliyedai kulipa ada kwa kipindi cha miaka tisa kwa ajili ya watoto wake wawili ikiwemo ada ya masomo, ada ya ukarabati, ada ya maendeleo,ada ya bima,vitabu,kalamu na tahadhari.

"Kwa muda wote mlalamikaji aliamini shule imesajiliwa kutoa huduma za bima na ina mpango mzuri wa huduma za bima kwa watoto wake wanapokuwa shuleni hadi siku mtoto wake (jina linahifadhiwa), aliporudi nyumbani akiwa amevunjika mguu bila kupatiwa huduma yoyote ya kimatibabu," amesema kamishna.

"Mzazi alipofuatilia kwa uongozi wa shule ili kujua hatua zilizochukuliwa na shule na kuuliza utaratibu wa bima, hakupata majibu ya kuridhisha na badala yake shule hiyo baadae iliwaondoa watoto wa mlalamikaji kusoma shuleni hapo hadi sasa hivi," ameongeza.

Amesema shule hiuo ilisajiliwa mwaka 2014 kwa namba ya usajili PS0102150 na kutoa huduma ya elimu kwa wanafunzi wa awali na msingi na kuanzia mwaka huo imesajili wanafunzi 181 wa elimu ya awali na wanafunzi 1,038 wa elimu ya msingi.

Kamishna huyo amesema ili kuwalinda walaji wa huduma za bima, ilipopokea malalamiko ya mzazi huyo ilichukua hatua ikiwa ni pamoja na kuandika barua shule hiyo kuhusu malalamiko hayo na kuomba kupata maelezo, ambapo mamlaka hiyo pia ilifanya ukaguzi kwenye shule hiyo.

Ametaja hatua nyingine ilikuwa ni kuitisha kikao ili kutatua tatizo hilo ambapo ilimwalika mzazi huyo na uongozi wa shule hiyo Septemba 13 na Oktoba 10,mwaka hii ila uongozi wa shule hiuo hawakufika wala kutuma mwakilishi.

"Mamlaka ili kulinda haki ya mkata bima (Oyage) inaelekeza shule kurudisha fedha iliyokusanywa kutoka kwa mzazi huyo kwa muda  wote watoto wake walipokuwa wanasoma shuleni hapo kwa kuwa ada hizo hazijatumika kutoa kinga aliyostahili na kulipa faini ya Sh5 milioni kwa mamlaka kutokana na kukusanya ada za bima bila kusajiliwa," amesema Kamishna

"Izingatiwe kwamba kushindwa kutekeleza maelekezo niliyotaja pamoja na  kulipa faini hiyo kwa mamlaka kutasababisha mmiliki wa Tanganyika kufunguliwa mashtaka (jinai) kwa mujibu wa kifungu 161(1) cha Sheria ya bima," amesisitiza.