Tani 254 za sukari zaanza kutua Mwanza, wafanyabiashara wataka bei iongezeke

Mfanyabiashara wa duka katika Mtaa wa Kamanga Feri jijini Mwanza akipima sukari kwa ajili ya mteja wake.  Picha na Mgongo Kiatira

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amewataka wauzaji wa sukari mkoani humo kutanguliza uzalendo wanapofanya biashara

Mwanza. Wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya jumla mkoani Mwanza wameiomba Serikali kupitia upya bei elekezi ya sukari iliyotolewa ya Sh140,000 kwa mfuko wa kilo 50 huku wakidai wakiuza kwa bei hiyo watapata hasara.

Kwa mujibu wa tangazo la Serikali Na. 40B lililotolewa Januari 23, 2024, kilo ya sukari katika mikoa ya kanda ya ziwa itauzwa kati ya Sh2,650 hadi 2,800 kwa bei ya jumla na Sh2,800 hadi Sh3,000 kwa bei ya rejareja.

Akizungumza leo Jumatatu Februari 26, 2024, katika kikao na wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya jumla, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema tani 254.5 za sukari zimeanza kutua.

Huku akiagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa bei elekezi ya Serikali kwa vitendo, Makalla amesema anatarajia kuona bei ya sukari ikishuka kutoka Sh4,000 kwa kilo, bei ya rejareja mtaani hadi Sh2,800 ili kuleta unafuu kwa wananchi.Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla (wa kwanza kulia) akiongoza kikao cha wafanyabiashara wa sukari jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira

“Bei elekezi ya jumla ya sukari imeshakokotolewa huko, ndiyo maana mliamua kununua sukari mliyoagiza kwamba sukari ukiuza jumla utaanzia Sh2,650 mpaka 2,800 na ukiuza rejareja ni Sh2,800 mpaka Sh3,000. Changamoto ya sukari inapotokea ni kero kwa wananchi,” amesema Makalla.

“Maelekezo yangu kwa wakuu wa wilaya ni kwamba washirikiane na maofisa biashara, siyo maofisa biashara wakae maofisini wakitoa leseni tu, pia changamoto za wateja na walaji wazishughulikie. Hatuna tena kisingizio sukari inapatikana sasa.”

 Makalla amesema atakuwa akiulizia hali ya upatikanaji wa sukari na bei zake huku akisema ahadi ya Serikali ni kuagiza sukari nje ya nchi hadi pale itakapotosheleza mahitaji ya wananchi.

Wakati Makalla akitoa maagizo hayo, mfanyabiashara, Monica Busumabu ameeleza kushtushwa na bei elekezi iliyotangazwa na Serikali akisema mbali na kuwasababishia hasara, inatishia uhai wao katika biashara.

Monica ambaye amethibitisha kuagiza shehena ya tani 31 za sukari, ameeleza kuuziwa mfuko wa kilo 50 kwa Sh140,000 na Kampuni ya Mohammed Enterprises (METL) jijini Dar es Salaam, huku akipendekeza waruhusiwe kuuza mfuko wa kilo hizo 50 jijini Mwanza kwa angalau Sh155,000.

Akijibu malalamiko hayo, Meneja wa METL Mkoa wa Mwanza, Roshan Ali amesema: “Tumekuwa na kikao kizuri na mkuu wa mkoa na tumepata changamoto zilizoibuliwa na nitaziwasilisha ofisini ili tuzipatie ufumbuzi ila sukari ipo na itapatikana kwenye kila duka.”

Hata hiyo, mfanyabiashara Monica ameendelea kusema kuwa, METL iliyopewa zabuni ya kuagiza sukari nje ya nchi, mbali na kuwauzia sukari kwa bei ya Sh140,000 jijini Dar es Salaam, pia inasafirisha hadi Mwanza na kuuza kwa wafanyabiashara wa kawaida kwa Sh150,000 jambo alilodai linaua soko la bidhaa yao.

“Tunaolangua kwake sukari Dar es Salaam, naye anasafirisha na kuuza bidhaa hiyo hiyo jijini Mwanza kwa wafanyabiashara wa kawaida kwa bei sawa na sisi. Tunaomba kama METL anatuuzia sisi kule Dar es Salaam basi asiruhusiwe kusafirisha na kuuza Mwanza ili kulinda mitaji yetu,” amesema Monica.

Mfanyabiashara mwingine wa sukari, Joyce Maduhu amekitaja kitendo cha METL kuwauzia sukari Dar es Salaam kisha kushindana nao katika soko la kawaida Mwanza ni unyonyaji unaolenga kuondoa ushindani na kuwafilisi mitaji yao.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amewataka wauzaji wa sukari kutanguliza uzalendo wanapofanya biashara ya bidhaa hiyo.

“Siyo kila biashara utapata faida, sasa leo huyu METL anaagiza, anauza nchi nzima kwa wafanyabishara wa jumla mikoani halafu anawafuata tena huko wanakopeleka, haiwezekani naomba awe mzalendo,” amesema Makilagi.


Madhara mitaani

Athari za bidhaa hiyo hazijamuacha salama mkazi wa Mkolani Mwanza, Restuta Zacharia ambaye amelazimika kufuta ratiba ya chai katika familia yake ili kukabiliana na makali ya ongezeko hilo.

“Nilienda dukani, nikakuta inauzwa Sh4,400 kwa kilo, mambo yamekuwa magumu kiasi kwamba nimelazimika kuondoa ratiba ya chai,” amesema Restuta.

Mamalishe wa Mtaa wa Kamanga Feri, Fausta Iseke amesema ongezeko la bei ya sukari limeshusha faida aliyokuwa anaipata kwenye biashara yake kutoka Sh30,000 hadi Sh5,000.

“Mimi napika chai na vyakula mbalimbali eneo hili la Kamanga, awali nilikuwa Napata faida hadi Sh30,000 kwa siku lakini sasahivi kutokana na kwamba chakula ninachouza kinatumia sukari kwa wingi, najikuta natumia gharama kubwa kununua sukari wakati bei ya chai wala chakula haijaongezeka,” amesema Feusta.

Mmiliki wa duka katika mtaa huo, Sauti Seiman, amesema idadi ya wateja wanaonunua sukari imeshuka kwa kuwa, awali alikuwa akitumia siku tatu kuuza kilo 25 za sukari, lakini sasa anatumia hadi wiki moja.

“Biashara ya sukari imedorora sijui watumiaji wamepungua? Hapa nauza kilo Sh4,000 lakini bado hawajitokezi kwa wingi kama ilivyokuwa awali, naomba Serikali iingilie kati suala hili kunusuru biashara na ustawi wa familia zetu,” amesema Seiman.