Tanroads kuanza ujenzi wa njia nne Arusha kukabiliana na msongamano

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe  akionyesha mtandao wa barabara itakayopanuliwa.

Muktasari:

 Mtandao wa barabara yenye urefu wa kilomita 9.3 itaanza kutandazwa kutoka eneo la Triple A’ itakayounganisha Barabara ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kuelekea mzunguko mkuu wa Kisongo


Arusha. Katika kukabiliana na msongamano wa magari Arusha, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umeanza mchakato wa ujenzi wa mtandao wa barabara ya njia nne kwa kiwango cha lami.

Mtandao wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 9.3 itaanza kutandazwa kutoka eneo la Triple A itakayounganisha Barabara ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kuelekea mzunguko mkuu wa Kisongo kupitia Barabara Kuu ya Dodoma.

Hayo yamebainishwa leo Machi 5, 2024 na Meneja wa Tanroad Arusha, Mhandisi Reginald Massawe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amesema barabara zinazoingia na kutoka Arusha kuelekea maeneo mbalimbali, zimeongeza msongamano, ndio maana wameamua kuanza mchakato mapema wa upanuzi wa barabara zake.

“Katika tathimini zetu, tumeona upo umuhimu wa kupanua njia zetu ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa magari na tumeanza na Barabara Kuu ya Dodoma itakayosaidia magari yanayotoka na kueleka mikoa ya kanda ya kati na ujenzi utaanza mara moja baada ya mchakato wa zabuni ulioanza hivi karibuni kukamilika,” amesema Massawe.

Amesema Tanroads pia inatekeleza miradi mikubwa ya barabara itakayounganisha Arusha na mikoa mingine ikiwamo ya urefu wa kilomita 453 itakayounganisha Jiji la Arusha na Wilaya ya Kongwa Dodoma kupitia wilaya za Simanjiro na Kiteto.

“Hii ni kwa ajili ya kufungua uwanda mkubwa za jamii ya wamasai ambayo uwezo wake wa kiuchumi umeanza kuonekana kutokana na ufugaji wa kisasa, kilimo na pia uwezekano mkubwa wa utalii,” amesema Massawe.

Barabara nyingine ni yenye urefu wa kilomita 339 itaunganisha miji ya Wilaya ya Karatu mkoani  Arusha na wilaya za Mbulu na Haydom mkoani Manyara na itatembea hadi Mto Sibiti, Singida  na Lalago hadi Maswa mkoani Simiyu.

Amesema kwa Arusha pekee kuna barabara yenye urefu wa kilomita 152 zilizoko katika hatua mbalimbali za ujenzi wa kiwango cha lami ikiwamo zile korofi za kuunganisha Mianzini na Ngaramtoni ya juu yenye kilomita 18, Karatu hadi Kilimapunda yenye kilomita 51 na Mbauda hadi Losinyai yenye urefu wa kilomita 28.

“Barabara nyingine ni ile ya Mto wa Mbu hadi Selela yenye urefu wa kilomita 23, Wasso hadi Loliondo yenye kilomita 10 na Packers hadi Losinyai yenye urefu wa kilomita 22 na hizi zote zinatarajia kukamilika mwaka huu na kurahisisha usafiri na biashara za mifugo na mazao,” amesema Massawe.

Akizungumzia mafanikio ya Tanroad Arusha kwa miaka mitatu, amesema hadi sasa wameongeza mtandao wa barabara za lami kwa kilomita 53, kutoka kilomita 425.78 zilizokuwapo mwaka 2021 hadi kilomita 478.78.

“Hii imetokana na bajeti ya Sh49 bilioni tuliyotengewa kwa miradi ya matengenezo ya barabara na madaraja na tumeshajenga madaraja makubwa mawili na mizani ya kupima magari iliyoko mpakani mwa Kenya na Tanzania eneo la Namanga wilayani Longido. Pia, tumelipa fidia zaidi ya Sh5.9 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja cha ndege Karatu,” amesema Mhandisi Massawe.

Ametaja madaraja hayo kuwa ni ya Nduruma lenye urefu wa mita 35 lililounganisha mawasiliano kati ya wananchi wa Usa River na Kijenge, lakini pia daraja la Kimosonu iliyosaidia wananchi wa mbuga za wanyama Arusha na wa kutoka Oldonyosambu lenye urefu wa mita 17.

Hivi karibuni, wakazi wa Arusha wamekuwa wakitoa maombi yao kwa Serikali juu ya upanuzi wa barabara zake kuu zinazoingia mjini kati ili kupunguza msongamano wa magari na ajali zinazotokea mara kwa mara.

Rehema Amos, mkazi wa Ngaramtoni amesema kuwa ufinyu wa barabara unachangia ajali.

“Hapa kungekuwa na barabara mbadala, magari mengine yangepita njia ya dharura lakini hakuna, hivyo Serikali ione ukuaji wa kasi wa mji wa Arusha wapanue barabara zake,” amesema.

Amos Mwita, amependekeza pia Barabara ya Namanga inayounganisha Kenya na Tanzania ipanuliwe, sambamba na ile ya Arusha Moshi kuanzia Usa River hadi Chuo cha ATC.