Tanroads Pwani watengeneza maeneo korofi tahadhari Elnino


Muktasari:

  • Matengenezo katika barabara kuu Pwani yanayohusisha kufukua madaraja kwenye sehemu za kuingilia na kutokea maji na kufukua makalvati yafanyika haraka ikiwa ni tahadhari ya Elnino.

Pwani. Katika kukabiliana na mvua za Elnino zilizotabiriwa kuonyesha Oktoba, Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani (Tanroads) imeanza na inaendelea kufanya matengenezo kinga katika barabara zake yanayohusisha kufukua maeneo ya madaraja kwenye sehemu za kuingilia na kutokea maji pamoja na kufukua makalvati katika barabara kuu zake za Chalinze/Segera/Manga, Morogoro na ile ya Kilwa road Kongowe hadi Malendego.

Kazi hiyo inafanyika baada ya kupata maelekezo ya Serikali kuhusu tahadhari ya mvua za elnino ambapo wakala hao walianza kwanza kufanya ukaguzi wa madaraja yake yote 318 na makalvati 1,540  za mkoani Pwani kama hatua ya awali inayolenga kujua uharibifu na namna ya uhitaji wa matengenezo ulivyo.

Meneja wa Tanroad Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage akizungumza  leo Oktoba 18 tahadhari waliyochukua ya mvua za elnino, ametaja  upande wa barabara ya Chalinze/Segera matengenezo yamefanyika katika daraja la Chalinze Mzee, Mazizi, Mkombezi, Kimange na makalvati madogo madogo ambayo yapo eneo la Manga.

Ikumbukwe kwa Mkoa wa Pwani barabara korofi zaidi ni ile ya Chalinze/Segera ambapo mara nyingi huko nyuma imekua ikitokea katika Daraja la Chalinze Mzee, Mazizi, Mkombezi na hivi karibu mwaka huu eneo la Kimange na maeneo ya vilimavilima jiran na eneo la Manga.

"Hii kitu inafanyika kuzuia kabisa uwezekano wa barabara kujifunga katika mwaka huu wa fedha na napenda kuwajulisha wananchi hatua hizi tunazochukua sasa tunaita hatua kinga ni hatua muhimu sana za awali ili kuzuia kabisa uwezekano wa maji kupita juu ya barabara na kumomonyoa kingo zake na hivyo kusababisha eneo kujifunga," amesema Meneja Tanroad Pwani.

Mhandisi Mwambage ameongeza kwa daraja la mto Ngerengere kazi hiyo ya matengenezo kinga pia imekamilika baada ya kufukua kipende cha mita 100 sehemu maji yanapotokea na mita 60 upande mwingine na kwamba pia imefanyika daraja la Mdaula, Msufini na Picha ya Ndege.

"Barabara ya Kilwa Road kwa maana ya Kongowe hadi Malendego sehemu kule sehemu inayosumbuaga  huwa ni daraja la Mwanambaya na na Daraja la Mto Ruhoi kwa hiyo kwa ujumla mpaka sasa tayari madaraja 20 yote yameshafunguliwa na makalvati yetu 1,540  yote  yameshafunguliwa,"amesema.

"Tanroad Pwani tunachoenda kufanya sasa kwa kipindi chote kile ambacho mvua itakua zikinyesha tutakuwa katika maeneo hayo na mengine yote yale tukihakikisha tunaangalia madhara yanayoendelea kujitokeza iwapo yatajitokeza kila siku na kuchukua hatua stahiki kulingana na tatizo litakavyokua linajitokeza," amesema.

Aidha akizungumzia matengenezo kuhusu Daraja la Lukigura linalounganisha Pwani na Morogoro kupitia Wilaya ya Bagamoyo na Mvomero Mhandisi huyo amesema ni uimarishaji sehemu ambayo maji hua yanadondokea na kupita eneo la daraja na kazi hiyo ipo mwishoni inatarajiwa kukamilika ndani ya siku nne adi tano kuanzia sasa.

Amewataka watumiaji wa barabara wakipita eneo lolote na kuona maji yanapita juu ya barabara watoe taarifa wasivuke kwanza wasubiri mpaka pale Tanroads itakapofanya utafiti na kuona eneo ilo ni salama na kuchukua hatua stahiki.

Katika mwaka wa fedha wa  2023/24 Sh18.980 bilioni ndiyo zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu, mkoa na madaraja mkoani Pwani ambapo Sh950  milioni ni kwa ajili ya matengenezo ya madaraja 318 na makalvati 1,540  hivyo

matengenezo kinga hayo yaliyofanyika ni sehemu bajeti hiyo.

Baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo ya madaraja hayo pamoja na madereva wameshukuru hatua hiyo ya Tanroads kuchukua tahadhari kwa kufanya matengenezo kinga kwa sababu wamekua wakikwama kuendelea na safari, kusafirisha mizigo, abiria na kupata hasara ya biashara huku wenyeji wakipoteza mazao mashambani.