Mmoja afariki Bukoba maadhara ya mvua yakiendelea Kanda ya Ziwa

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Rwamishenyi Manispaa ya Bukoba wakiangalia baadhi ya nyumba zilizoezuliwa paa baada ya mvua iliyoambatana na upepo mkali kunyesha mjini Bukoba alfajiri ya kuamkia Oktoba 18, 2023. Picha na Alodia Dominick

Muktasari:

Madhara ya mvua yameanza kuriptowa siku kadhaa baada ya tahadhari ya mvua za El Nino iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) huku mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwa katika orodha ya maeneo yaliyotajwa kwenye tahadhari hiyo ya Oktoba 6, 2023.

Bukoba. Mvua iliyoambatana na upepo mkali umesababisha kifo cha mtu mmoja huku nyumba zaidi ya 100 yakiezuliwa paa mjini Bukoba.

Wakazi wa Kata za Rwamishenyi, Hamugembe na Kashai ndio wameathiri zaidi katika janga hilo lililotokea alfajiri ya Oktoba 18, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 18, 2023,

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amewaambia Waandishi wa habari leo Oktoba 18, 2023 kuwa mtu aliyepoteza maisha katika tukio hilo hajatambulika na mwili wake ulikutwa mtaroni.

‘’Vyombo vya dola kwa kushirikiana na wataalam wa afya wanafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu ya kifo cha mtu huyo baada ya mwili wake kukutwa na jeraha kwenye paji la uso linaloashiria ama kujibamiza au kupigwa na kitu kizito,’’ amesema Siima ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya wilaya

Amesema tathmini ya awali umebaini kuwa miongoni mwa nyumba zilizoezuliwa paa ni makazi ya watu, nyumba za taasisi za umma kama shule, kituo cha afya na kanisa.

Padre Egidius Rweyemamu amesema Kanisa Katoliki Parokia ya Rwamishenyi ni miongoni mwa nyumba za ibada zilizoezuliwa paa katika tukio lililoawaacha waumini wawili wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini.

Diwani wa Kata ya Rwamishenyi, Sued Kagasheki amesema japo tathmini bado inaendelea, madhara ya mvua hiyo kwenye kata hiyo inaonekana zaidi katika mitaa Kamizilente, National Housing na Rwamishenye.

Athari za mvua ya upepo zinashuhudiwa Manispaa ya Bukoba siku chache tangu wakazi wa tarafa za Nyang’wale na Nyijundu Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita kupata madhara kama hayo ambayo pia yalisababisha kifo mtu mmoja huku nyumba kadhaa zikiezuliwa paa.

Tukio hilo la Nyang’wale lilitokea Oktoba 15, 2023 ambapo Katibu Tawala Wilaya ya Nyang’wale, Kaunga Amani aliiambia Mwananchi kuwa pamoja na makazi ya watu, nyumba za taasisi za umma pia ziliezuliwa.

Madhara ya mvua yameanza kuriptowa siku kadhaa baada ya tahadhari ya mvua za El Nino iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) huku mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwa katika orodha ya maeneo yaliyotajwa kwenye tahadhari hiyo ya Oktoba 6, 2023.