Tanroads wapiga kambi Mlima Kitonga kuondoa mawe barabarani

Shughuli ya uondoaji wa mawe yanayoporomoka kutoka mlimani ikiendelea.

Muktasari:

Watendaji wa Wakala wa Barabara mkoani Iringa wameweka mkakati wa kuhakikisha wanaondoa mawe yanayoporomoka kutoka katika Mlima Kitonga na Nyang'oro ili kuepusha ajali.

Iringa. Watendaji wa Wakala wa Barabara mkoani Iringa wameweka mkakati wa kuhakikisha wanaondoa mawe yanayoporomoka kutoka katika Mlima Kitonga na Nyang'oro ili kuepusha ajali.

Nyang'oro na Kitonga ni milima yenye kona kali katika barabara za Iringa - Dodoma na Iringa -Dar es Salaam.

Moja ya changamoto zinazoikabili milima hiyo ni uwepo wa miamba ya mawe ambayo kipindi cha mvua hasa za El nino imekuwa ikiporomoka na kusababisha ajali.

Kwa sasa Tanroads wanafanya matengenezo ya barabara kwenye mlima Kitonga ili kupunguza ukali wa kona kwenye baadhi ya maeneo,  ambazo zimekuwa zikisababisha msongamano wa magari.

Akizungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Meneja wa Tanroads Mkoani Iringa,  Yudas Msangi amesema mkakati wa kuondoa mawe hayo umesaidia kuepusha ajali.

"Kitonga ina kona nyingi lakini kona kali ni zaidi ya 20, kutokana na mvua za El nino kumekuwa na mawe yanapoporomoka kutoka juu. Tumekuwa tukiyaondoa haraka sana," amesema na kuongeza:

"Kwenye hizo kona 20 suluhisho la haraka imekuwa ni kufanya matengenezo kwa gharama ya Sh6.4 bilioni," amesema.

Amesema pia wameweka vioo vikubwa kwa ajili wa kuwasaidia madereva kuona upande wa pili wa barabara kwenye maeneo ya kona.

Baadhi ya madereva wa mabasi na magari ya mizigo wamesema kuporomoka kwa mawe kwenye mlima huo ni kati ya changamoto zinazosababisha ajali ya mara kwa mara.

"Ilishatokea nafika tu kwenye kona jiwe kubwa linaanguka, nashukuru niliweza kulikwepa. Niwapongeze Tanroads kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwenye huu mlima." amesema Linus Ndeya, dereva wa lori.

Kwa upande wake,  msimamizi wa kitengo cha matengenezo Tanroads Mkoa wa Iringa, Bokeye Marwa mbali na Kitonga, mvua za El nino zimeathiri barabara za Kibena - Idete, Nzihi - Idodi, Msembe na Kidabaga ambazo tayari zimeshatengenezwa.