Tanzania, Japan kushirikiana katika uhifadhi wa urithi wa dunia
Muktasari:
- Makubaliano hayo yamefikiwa leo Julai 22, 2026 jijini Busani, Korea Kusini kati ya Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Unesco, Said Yakubu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Iwao Horii, pembezoni mwa kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco kinachoendelea jijini humo.
Dar es Salaam. Tanzania na Japan zimekubaliana kuimarisha ushirikiano baina yao katika maeneo ya uhifadhi wa urithi wa dunia, utamaduni na maendeleo endelevu kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Julai 22, 2026 jijini Busani, Korea Kusini kati ya Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Unesco, Said Yakubu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Iwao Horii, pembezoni mwa kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco kinachoendelea jijini humo.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Horii ameambatana na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Japan katika Unesco, Mheshimiwa Takehiro Kano.
Balozi Yakubu ameishukuru Serikali ya Japan kwa mchango wake katika kuhifadhi urithi wa utamaduni nchini Tanzania, hususan kupitia ufadhili wa ukarabati wa Jumba la Sinema la Majestic, Zanzibar.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Said Yakubu (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Iwao Horii (wa tatu kushoto), baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika pembezoni mwa kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco kinachoendelea jijini Busani, Korea Kusini.
Aidha, ameipongeza Japan kwa kuendelea kuunga mkono miradi ya uhifadhi wa maeneo ya urithi wa dunia barani Afrika, hatua hiyo imekuwa na mchango muhimu katika kulinda historia, utamaduni na urithi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mazungumzo hayo, pia, yalijikita katika fursa za kupanua ushirikiano kupitia programu za kujengea uwezo wataalamu wa urithi, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pamoja na kuendeleza miradi ya pamoja ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa maeneo ya urithi wa dunia nchini Tanzania.
Balozi Yakubu amemkaribisha Horii kutembelea Tanzania ili kujionea maeneo mbalimbali ya urithi wa dunia yaliyosajiliwa na Unesco pamoja na fursa zilizopo katika sekta ya utamaduni na urithi.
Katika kikao hicho, Balozi Yakubu aliambatana na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Taifa ya Unesco Tanzania, Profesa Hamisi Malebo, pamoja na maofisa wengine waandamizi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania unaoshiriki Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia.
Kikao hicho kinaendelea hadi Julai 29, 2026, kikijadili masuala yanayohusu ulinzi, uhifadhi na usimamizi endelevu wa maeneo ya urithi wa dunia, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kulinda urithi wa asili na wa utamaduni kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.