TIB Rasilimali, Orbit Securities kusaidia upatikanaji wa mitaji
Mkurugenzi Mkuu wa TIB Rasilimali, Brighton Kinemo (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Orbit Securities Limited, Godfrey Malauri wakionesha mkataba wa makubaliano ya kimkakati yanayolenga kurahisisha upatikanaji wa fedha kupitia soko la mitaji.
Muktasari:
- Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha soko la mitaji nchini kwa kuongeza ushirikiano, kuvutia wawekezaji, kupanua fursa za kifedha na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania.
Dar es Salaam. Wakati upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu ukiendelea kuwa changamoto kwa kampuni nyingi na taasisi zinazotekeleza miradi mikubwa nchini, TIB Rasilimali Limited na Orbit Securities Limited wameingia makubaliano ya kimkakati yanayolenga kurahisisha upatikanaji wa fedha kupitia soko la mitaji.
Makubaliano hayo yanakusudia kuunganisha uzoefu na uwezo wa taasisi hizo mbili ili kutoa suluhisho bunifu za kifedha kwa wateja wa sekta binafsi na umma jambo litakalochochea kuongeza fursa kwa kampuni za umma na binafsi kupata fedha za kuendesha na kupanua shughuli zao.
Akizungumzia ushirikiano huo Mkurugenzi Mkuu wa TIB Rasilimali, Brighton Kinemo amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na kampuni binafsi zinazotafuta fedha za kutekeleza miradi mikubwa kupitia soko la mitaji nchini Tanzania.
Mbali na kuongeza mitaji, makubaliano hayo yanakusudia kuimarisha imani ya wawekezaji, kupanua ushiriki katika soko la mitaji, kuongeza fursa za uwekezaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha.
“Makubaliano haya ni dhamira ya taasisi katika kupanua upatikanaji wa suluhisho bunifu za soko la mitaji kwa maendeleo ya uchumi kwani kwa kuunganisha utaalamu kutasaidia kujenga jukwaa imara litakalowezesha taasisi za umma na binafsi kupata njia bora, bunifu na endelevu za kufadhili miradi yao ya maendeleo,” amesema.
Amesema ushirikiano huo pia utaongeza thamani kwa wateja kupitia huduma zenye ubora mkubwa huku ukichangia kuimarisha maendeleo na ushindani wa soko la mitaji nchini Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Orbit Securities Limited, Godfrey Malauri amesema ushirikiano huo umeziweka taasisi hizo katika nafasi nzuri ya kutoa huduma bora zaidi za ushauri wa kifedha na uhamasishaji wa mitaji.
Amesema lengo lao ni kuongeza thamani kwa wateja, kuendeleza uwekezaji, kuhimiza ubunifu na kuharakisha mageuzi ya kiuchumi kupitia matumizi ya suluhisho madhubuti za masoko ya mitaji nchini Tanzania.
“Makubaliano haya yatachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano kupitia uwekezaji na upatikanaji wa mitaji,” amesema.