Tanzania, Msumbiji kushirikiana sekta za uchumi

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine
Muktasari:
Tanzania imekutana na Msumbiji kufanya tathmini ya ushirikiano katika sekta ya elimu, maji, ujenzi na usafirishaji.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imekutana na Msumbiji kufanya tathmini ya makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa 14 kuhusu ushirikiano katika sekta za elimu, maji, ujenzi na usafirishaji.
 Makubaliano hayo yalifikiwa mwaka 2006 katika mkutano huo uliolenga kuimarisha maeneo ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza leo Jumatatu, Agosti 22, 2022 katika mkutano wa 15, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amesema mbali na tathmini pia wanatarajia kujadili fursa mpya.
"Tumeanza mikutano ya tume ya pamoja na leo tutafanya tathmini ya makubaliano tuliyofikia katika mkutano wa mwisho wa mwaka 2006," amesema.
Balozi Sokoine amefafanua kwa sababu ni miaka 16 imepita tangu ufanyike mkutano huo, yulimwengu imebadilika hivyo mambo mengine yanatarajiwa kujadiliwa.
Ameeleza katika mkutano wa leo fursa za ushirikiano katika sekta ya elimu, maji, umwagiliaji, kilimo, uvuvi na uchumi wa buluu zitajadiliwa kisha baadaye kusaini mikataba ya ushirikiano.