Tanzania mwenyeji mkutano wa COP12, mafanikio yanatarajiwa
Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuangaza rasmi kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), utakaofanyika Oktoba 6 hadi 9, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Picha na Mbonea Herman.
Muktasari:
- Serikali imetangaza kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) utakaofanyika Oktoba mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Tanga. Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) utakaofanyika Oktoba 6 hadi 9, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa leo Julai 2, 2026 jijini Tanga na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini humo.
Amesema Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, inaonyesha imani kubwa ambayo jumuiya ya kimataifa imeiweka kwa Taifa hili katika kusimamia hifadhi ya mazingira ya bahari na ukanda wa pwani.
Amesema mkutano huo utakutanisha nchi wanachama kujadili utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi, kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari, kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuendeleza uchumi wa buluu unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
“Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa COP12, hatua inayodhihirisha nafasi yake katika uongozi wa uhifadhi wa mazingira ya Bahari ya Hindi na kufungua fursa mpya za uwekezaji, ushirikiano wa kimataifa na maendeleo ya uchumi wa buluu,” amesema Kwagilwa.
Naibu Waziri huyo amesema mkutano huo, pia, utaangalia masuala ya urejeshaji wa mifumo ikolojia ya bahari, ikiwemo mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi bahari pamoja na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa inayolenga kulinda bioanuai za bahari.
Amebainisha kuwa Serikali tayari imeunda kamati za kitaifa kwa kushirikiana na wizara, taasisi za umma, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha maandalizi yote yanakamilika kwa wakati na mkutano unafanyika kwa mafanikio makubwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda amesema maandalizi ya mkutano huo yameanza huku yakilenga kuhakikisha Tanzania inanufaika na fursa za kidiplomasia, kiuchumi na kitaalamu zitakazotokana na mkutano huo.
“Tunatarajia kupokea washiriki kati ya 500 na 600 kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi pamoja na taasisi za kimataifa. Hivyo maandalizi ya kina ni muhimu ili kuhakikisha Tanzania inaandaa mkutano wenye viwango vya kimataifa,” amesema Balozi Luvanda.
Ameeleza kuwa mkutano huo utatoa nafasi ya kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za mazingira ya bahari, kuongeza ushirikiano wa kikanda na kuweka mikakati mipya ya matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani amesema matokeo ya utafiti uliofanyika mkoani humo yanaonyesha athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji, hususan kilimo cha mwani.
“Tumeshuhudia ongezeko la karibu nyuzi joto tatu baharini, huku siku za wavuvi kwenda kuvua zikishuka kutoka 221 mwaka 2021 hadi 170 kutokana na upepo mkali na hatari ya usalama baharini. Pia, mavuno ya samaki yamepungua kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30,” amesema Dk Buriani.
Amesema takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia ushirikiano wa kikanda na kimataifa, akieleza kuwa uenyeji wa COP12 utaipa Tanzania jukwaa muhimu la kujadili suluhisho za kisayansi na sera zitakazosaidia kulinda mazingira ya bahari na kukuza uchumi wa buluu kwa maendeleo endelevu.