Tanzania yaanza utafiti wa chanjo mpya ya Malaria

Muktasari:

  • Wakati mapema wiki hii dunia ikiandika historia ya kupata chanjo ya ugonjwa wa Malaria kwa watoto, Tanzania imeanza utafiti wa chanjo ya majaribio R21 itakayohusisha watoto 600.


Dar es Salaam. Wakati mapema wiki hii dunia ikiandika historia ya kupata chanjo ya ugonjwa wa Malaria kwa watoto, Tanzania imeanza utafiti wa chanjo ya majaribio R21 itakayohusisha watoto 600.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya chanjo ya awali RTS,S iliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Ifakara Health Institute (IHI) kwa miaka 15 huku ikihusisha watoto 4000, kuidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mtafiti kiongozi kutoka IHI, Dk Ally Olotu alilieleza Mwananchi jana kuwa chanjo hiyo mpya ya R21 iliyotengenezwa na watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford na Burkina Faso, imeonekana kuwa na ufanisi wa asilimia 77 katika majaribio ya awamu ya pili.

“Tanzania tumeipokea na tumeanza rasmi majaribio kwa awamu ya tatu ambapo watoto 600 watashiriki katika utafiti huu unaoendelea Kiwangwa Bagamoyo, pia utashirikisha jumla ya watoto 5000, ambapo wengine ni kutoka mataifa ya Mali, Burkina Faso, Kenya na Tanzania na utakamilika baada ya miaka miwili.

“Chanjo iliyopatikana RTS,S ni mafanikio makubwa lakini bado haina nguvu sana, tumekuwa tukitafuta chanjo kwa zaidi ya miaka 35 hatuishii hapo, lazima utafiti uendelee kutafuta chanjo iliyo bora zaidi. Hii imeonyesha ubora kwa asilimia 77 hivyo tunaendelea kutafiti,” alisema Dk Olotu.

Alisema Tanzania ilishiriki katika hatua ya pili na tatu ya chanjo iliyofanikiwa na ilikuwa miongoni mwa nchi sita kutoka barani Afrika zilizoshiriki.

“Mwaka 2009 ulihusisha watoto 16,000 na kwa Tanzania tulifanyia Bagamoyo na Korogwe, Tanga ambapo watoto 4000 walishiriki matokeo ya ule utafiti, matokeo ni salama na pili ina uwezo wa kukinga kwa asilimia 40 kwa ugonjwa wa kawaida na malaria kali kwa asilimia 30,” alisema.

Alisema baada ya utafiti huo, WHO ilihitaji ufanywe kwa watu wengi zaidi na ndipo ulipoenda kufanywa katika nchi za Ghana, Malawi na Kenya kwa watoto 800,000.

Chanjo ya RTS,S

RTS,S ni chanjo inayofanya kazi dhidi ya vimelea vinavyoambukizwa na mbu (Plasmodium falciparum), ambavyo ni vimelea hatari zaidi ulimwenguni na vilivyoenea barani Afrika.

Kwa upande wa Afrika, ambapo Malaria inaua zaidi ya watoto 260,000 walio chini ya umri wa miaka mitano kila mwaka, chanjo hii ni imeleta matumaini, hasa wakati hofu ya kujizatiti kwa malaria dhidi ya matibabu ikiongezeka.

“Kwa karne nyingi, malaria imeshambulia ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na kusababisha mateso makubwa,” alisema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO katika kanda ya Afrika.

“Tumetarajia kwa muda mrefu kupata chanjo ya malaria inayofaa na sasa kwa mara ya kwanza, tuna chanjo iliyopendekezwa kwa matumizi,” aliongeza.

Tangu mwaka wa 2019, nchi tatu za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Ghana, Kenya na Malawi, zilianza kutumia chanjo hiyo katika maeneo yaliyochaguliwa ambapo maambukizo ya malaria yamekuwa yakiongezeka.

Mapema wiki jana, watafiti na wataalamu wa afya walisherehekea hatua ya Shirika la Afya Duniani kuidhinisha matumizi wa chanjo ya kwanza ya malaria.

Utengenezaji wa chanjo za malaria ni mchakato mrefu kwani ni ugonjwa ambao ni vigumu kukabiliana nao ukilinganisha na Uviko-19.

RTS,S ni chanjo ya kwanza ya malaria ambayo imepitia hatua zote zinazohitajika na kufanyiwa majaribio, lakini WHO inasema chanjo ya pili ya malaria inaweza kuwa na faida kubwa kwa udhibiti wa malaria” kwani itasaidia kukidhi mahitaji makubwa yanayotarajiwa.

Hata hivyo, bado kuna maswali mengi, kwa kuwa takwimu zinaonyesha zaidi ya watoto 260,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano hufariki kutokana na malaria kila mwaka katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na ni lini watoto wataanza kunufaika na chanjo hiyo lakini pia ni bora kwa kiasi gani?

Katika zaidi ya vimelea 100 vya malaria, baada ya kufanikiwa kwa mipango ya chanjo ya majaribio ya RTS, S nchini Ghana, Kenya na Malawi, WHO imesema chanjo hiyo inapaswa kusambazwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na katika maeneo mengine yenye maambukizi ya wastani na ya juu ya ugonjwa wa malaria.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema: “Ni wakati wa kihistoria. Imesubiriwa kwa muda mrefu kwa watoto ni mafanikio ya sayansi, afya ya mtoto na udhibiti wa malaria duniani, itaokoa maelfu ya watoto.”

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale alisema pamoja na chanjo ya RTS,S kuidhinishwa na WHO, Tanzania inabidi ijiridhishe kama ulivyo utaratibu.

Hata hivyo, wakati chanjo hiyo ikielezwa kuwa na ufanisi wa kinga kwa asilimia 40 na asilimia 30, WHO imesema ni hatua muhimu na njia ya ugunduzi wa chanjo zenye nguvu zaidi.

Chanjo hiyo, iliyotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya GSK, haitakuwa mbadala wa hatua nyingine zote za kudhibiti malaria kama vile vyandarua vilivyotibiwa na dawa za kuua wadudu.

Itatumika pamoja nazo ili kufikia lengo la kuzuia kabisa vifo vinavyotokana na malaria na haitatumika nje ya Afrika ambapo kuna aina tofauti za malaria, ambazo chanjo hiyo haiwezi kutumika kama kinga.