Tanzania yaimarisha timu ya kukabiliana na magonjwa ya dharura, mlipuko
Timu ya Kitaifa ya Matibabu ya Dharura na Milipuko (EMT) wakiwa katika kikao wakisikiliza hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Maafa, Dk. Erasto Sylvanus. Picha na Hamida Shariff
Muktasari:
- Endapo yatatokea magonjwa yoyote ya dharura au mlipuko timu hiyo ndiyo itakuwa mstari wa mbele kukabiliana nayo kwa haraka kupunguza vifo.
Morogoro. Tanzania ipo tayari kukabiliana na ugonjwa wa Ebola pamoja na magonjwa mengine ya milipuko baada ya kuandaa timu ya wataalamu wenye uwezo na utayari wakati wowote wa kukabiliana na magonjwa hayo.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Juni 12 na ofisa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Janeth Masuma, wakati wa kufunga mafunzo kwa timu ya matibabu ya magonjwa ya dharura na mlipuko (EMT) mkoani Morogoro.
Dk Janeth amesema endapo yatatokea majanga yoyote ya kiafya timu hiyo ndiyo itakuwa mstari wa mbele kukabiliana na majanga hayo kwa haraka na hivyo kupunguza vifo.
"Tanzania ni nchi ya 27 Afrika kuanzisha timu ya kitaifa ya magonjwa ya dharura na mlipuko, na Sasa timu hii ipo thabiti kukabiliana na magonjwa yoyote ya dharura," amesema Masuma.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo kutoka kitengo cha dharura na maafa Wizara ya Afya, Dk Erick Richard, amesema mafunzo hayo yalianza mwaka jana kutokana na utaratibu uliowekwa na WHO katika utoaji wa huduma za dharura na kwamba timu hiyo haitakuwa ya kitaifa tu, bali inaweza kutumika hata nje ya nchi endapo itahitajika.
Kwa mujibu wa Dk Richard mbali ya timu hiyo ya kitaifa kutoa matibabu ya magonjwa ya dharura na mlipuko, lakini pia itakwenda kuimarisha timu za magonjwa hayo kwenye taasisi zao za afya wanazotoka.
Naye mwenyekiti wa mafunzo hayo, Dk Hussein Manji, ametaja makundi ya waliopo kwenye timu hiyo ya kitaifa kuwa ni pamoja na wataalamu kutoka hospitali binafsi na Serikali wakiwemo wauguzi, madaktari mbalimbali na taasisi nyingine zinazoshughulika na masuala ya afya.
"Kama nchi sasa tunayo timu ya kukabiliana na magonjwa ya dharura itakayokuwa na kazi ya kudhibiti na kutoa matibabu, timu ambayo ina wataalamu wa afya kutoka vitengo mbalimbali vinavyohusika na masuala ya afya," amesema Dk Manji.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Maafa kutoka katika wizara hiyo, Dk Erasto Sylvanus, amesema Serikali imejitahidi kuimarisha mifumo ya utayari wa kukabiliana na magonjwa ya dharura na milipuko.
Dk Sylvanus amesema kupitia mifumo hiyo kunaweza kuwa na orodha ya magonjwa ya dharura yanayoweza kutokea, wakati gani yatatokea na namna gani ya kukabiliana nayo.
"Ikitokea ugonjwa wowote tunajua kabisa tunayo timu ya kudumu ya kukabiliana na ugonjwa huo na hii timu imejengewa uwezo wa kufanya kazi popote iwe ndani ama nje ya nchi, ," amesema Dk Sylvanus.
Katika maagizo yake, Mkurugenzi huyo amezitaka timu hiyo kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kuimarisha uwezo wa taasisi wanazotoka ili kuwa na timu ya dharura kwenye taasisi hizo, kuendelea kuzingatia viwango vya kimataifa ili kuweza kuwa na timu inayotambulika kikanda na kimataifa.
Agizo jingine alilolitoa ni timu hiyo kufanya kazi pamoja bila ya kujali taasisi wanazotoka wataalamu hao, kuwa wazalendo na kuwa tayari kufanyakazi wakati wowote na mahali popote Kwa harakanza.