Tarangire yataifisha ng’ombe 3,083 waliokutwa hifadhini

Ngombe wakiwa katika  hifadhi ya seerengeti mkoani Mara.Picha Maktaba

Muktasari:

  • Ukamataji mifugo inayoingia maeneo yaliyohifadhiwa kufuata malisho umeendelea kuacha kilio kwa wafugaji kwa ng’ombe 3,083 kutaifishwa baada ya kukamatwa kutokana kuingizwa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Arusha. Ukamataji mifugo inayoingia maeneo yaliyohifadhiwa kufuata malisho umeendelea kuacha kilio kwa wafugaji kwa ng’ombe 3,083 kutaifishwa baada ya kukamatwa kutokana kuingizwa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Ng’ombe hao wenye thamani zaidi ya Sh1.5 bilioni, walikamatwa jana na wanatarajiwa kuuzwa kwa mnada kama ilivyotokea maeneo mengine walikokamatwa baada ya kuingia hifadhini.

Ng’ombe hao waliokamatwa Tarangire wanamilikiwa na wafugaji wakazi wa Wilaya ya Simanjiro katika Mkoa Manyara na hadi jana wafugaji sita walikuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuingiza mifugo hiyo.

Kumekuwa na ongezeko la mifugo kuingia maeneo ya hifadhi ili kutafuta malisho kutokana na maeneo mengi nchini kukabiliwa na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Hadi jana, zaidi ya ng’ombe 7,000 walikuwa wamekamatwa baada ya kuingizwa katika maeneo ya hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na mashamba ya wakulima kusaka malisho.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mathew Mombo alisema ng’ombe hao wamekamatwa katika operesheni iliyoendeshwa kati ya Desemba 17 hadi 24 mwaka huu.

Mombo alisema mifugo hiyo, imekamatwa pembezoni mwa hifadhi maeneo ya Lebosiret na Chuki ambako bado kuna makundi ya mifugo yakitaka kuingizwa hifadhini.

“Tunawaonya wafugaji kuacha mara moja mipango yao ya kutaka kuingiza mifugo hifadhini kwani tutaendelea kuikamata na kuchukuwa hatua kali,” alisema Mombo.

Alisema operesheni za kukamata mifugo zitaendelea kufanywa katika hifadhi hiyo kwa kuwatumia askari na ndege za Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kuhakikisha wanyamapori wanakuwa salama na kuendelea kupata malisho.

“Tunaonya mifugo ambayo itakamatwa, itafikishwa mahakamani na kuuzwa kwa mnada kwani kuwapiga faini wafugaji haijaleta suluhu,” alisema.

Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Wizi wa Mifugo, Simon Pasua alisema wafugaji sita wanashikiliwa na polisi kutokana na kuingiza mifugo hifadhini ambao ni Murio Likasi, Moringe Mpeleke, Sabaya Suluni, Lebusi Laika, Terengo Koneki na Saluni Lesiro.


Wafugaji waiangukia Serikali

Baadhi ya wafugaji na wakurugenzi wa mashirika ya kutetea haki za binaadamu na wafugaji, waliiomba Serikali kuwasamehe wafugaji hao kwani wanakabiliwa na hali ngumu kutokana na kukosa malisho katika maeneo mengi waliyoyazoea.

Lenani Seyani, mmoja wa wafugaji hao, aliiomba Tanapa na Serikali kuwasaheme na kuwarejeshea mifugo yao kwani wana mahusiano ya muda mrefu na hifadhi.

“Sisi na hifadhi sio maadui, kipindi hiki wanyamapori wameanza kuja kwa wingi maeneo yetu ya makazi huku Terati na kwingineko na tumekuwa hatuwadhuru licha ya kuja na magonjwa,” alisema.

Mkurugenzi wa Shirika la Integrated Development Initiative in Ngorongoro (Idingo), Loseria Maoi aliiomba Serikali kuimarisha ujirani mwema na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi na kutoa elimu kwao ili kuepuka migogoro ikizingatiwa kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi yamesababisha ukame kwa muda mrefu hivyo kukosa malisho ya uhakika kwa mifugo yao.

“Tunaiomba Serikali kuwafikiria wananchi wake kwani wanabaki masikini kutokana na mifugo yao kupigwa mnada. Kwa mfano, Desemba 14, ng’ombe 1,772 mali ya wafugaji wa Loliondo Wilaya ya Ngorongoro waliuzwa kwa mnada wa hadhara kwa amri ya mahakama kwa madai kuwa mifugo hiyo haina mwenyewe na kuziacha kaya zaidi ya 22 zikiwa masikini,” alisema Maoi.

Mkurugenzi wa Shirika la PALISEP, Robert Kamakia alisema ni muhimu Serikali kuwasaidia wananchi kwa kutengeneza mifumo rafiki inayoweza kutatua changomoto zilizopo baina ya hifadhi za Taifa na wafugaji wanaozunguka maeneo hayo jambo litakalowawezesha kuendelea na shughuli zao bila kuingilia maeneo ya mamlaka.