Tarura Meatu kuachana na madaraja ya chini

New Content Item (1)
New Content Item (1)

What you need to know:

Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu imeanza kuachana na ujenzi wa madaraja ya chini (drift) kwa kujenga madaraja ya juu kuwezesha barabara za wilaya hiyo kupitika kipindi chote cha mwaka.

Meatu. Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu imeanza kuachana na ujenzi wa madaraja ya chini (drift) kwa kujenga madaraja ya juu kuwezesha barabara za wilaya hiyo kupitika kipindi chote cha mwaka.

Akizungumza leo Mei 2, 2023 wakati wa ziara ya ukaguzi wa barabara zilizofunguliwa mwaka 2022/23, Msanifu wa Ujenzi kutoka Tarura Wilaya ya Meatu, Maduhu Vicent amesema uamuzi huo umefikiwa kutokana na hali halisi ya mazingira ya mito wilayani humo.

"Mkondo wa mito inayopitisha maji mengi nyakati za masika hufunga njia na hivyo kukwamisha shughuli za usafirishaji hadi maji yanapopungua. Ujenzi wa madaraja ya juu utaondoa tatizo hilo," amesema Maduhu.

Amesema hadi sasa, Tarura inatekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja ya juu 20 kuboresha usafirishaji wilayani Meatu baada ya Serikali kufungua mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 1, 041.17 kati ya hizo, kilomita 85 zikiwa ni za barabara mpya.

“Tunatarajia kufanya ufunguzi wa kilomita 40 za barabara kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024,” amesema Maduhu

Jama John, mkazi Sakasaka wilayani Meatu amesema ujenzi wa madaraja ya juu siyo tu itarahisisha usafirishaji kipindi chote cha mwaka, bali pia itamaliza matukio ya watu na mali kusombwa nyakati za masika.

"Baadhi ya watu hukosa uvumilivu kwa kuhindwa kusubiri pindi maji yanapoongezeka juu ya madaraja ya chini; wengi hulazimisha kupita na mwishowe uhatarisha usalama wa maisha na mali zao kwa kusombwa na maji,” amesema Jama.

Kauli kama hiyo pia imetolewa na Masanja Ngeme, mkazi wa Mwakisandu akiongeza kuwa kupitika kwa barabara kipindi chote cha mwaka siyo tu itarahisisha usafirishaji, bali pia itapunguza bei ya bidhaa na mahitaji mbalimbali kutokana na kupungua kwa gharama za usafirishaji.