Tarura yasitisha faini tozo maegesho ya magari

Muktasari:

  • Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), umesitisha kwa muda utozaji wa faini za tozo za maegesho ya magari, baada ya kupokea mapendekezo na maoni ya wadau waliotaka kuongezwa muda wa elimu kuhusu mchakato huo. 


Dar es Salaam. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), umesitisha kwa muda utozaji wa faini za tozo za maegesho ya magari, baada ya kupokea mapendekezo na maoni ya wadau waliotaka kuongezwa muda wa elimu kuhusu mchakato huo. 

Mchakato wa kutoza faini tozo za maegesho kwa njia ya mtandao ulianza rasmi Machi 15, 2022 kwa watumiaji wa maegesho ya Tarura kutakiwa kulipa faini hiyo baada ya kupitisha siku 14.

Lakini baada ya Tarura kuanza kutoza faini hizo, kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa watumiaji wa maegesho hayo wakidai kutozwa faini kubwa, tofauti na kiwango cha deni linalodaiwa baada ya kupitisha muda wa kulilipa.

Wananchi hao wametoa malalamiko yao katika mitandao mbalimbali kijamii ukiwemo wa Twitter huku wakiomba ufafanuzi kutoka Tarura na kuhoji wamewakosea nini

“Jamani @TaruraTz tunaomba ufafanuzi katika hili, kama tumewakosea tuhame na hii nchi kabisa, gari yangu natoka home (nyumbani) naegesha kazini jioni narudi home, leo hii eti nadaiwa 49,000? gari ya mume wangu inadaiwa 162,500. Huku mafuta yamepanda, tutajenga kweli? Nimeumia tu,” ameandika Mrs Mrusi

Hancy Machemba ameandika “yaani kila baada ya siku mbili unampiga mtu fine (adhabu) Huu utaratibu gani? hata fine ya polisi baada ya muda fulani na sio siku mbili. Kwa kweli Tarura hapa mnatupiga na hizi pesa wala hazijulikani zinakwenda wapi, tuambieni ukweli na uwazi fine ni baada ya muda gani wa deni?

Wakati hao wakieleza hayo @Irontai ameandika yaani huyu toka Disemba anadaiwa 49k, (49,0000) ila mie wa mwezi wa tatu nadaiwa 83k  (83,0000).kweli?


Lakini katika taarifa hiyo, kupitia ukarasa wao Tarura walimjibu kuwa “tangu 15 Desemba 2021 hujawahi kufanya malipo ya maegesho Kidigitali. Ulikuwa unadaiwa Sh9, 000 hujalipa deni ambalo limepelekea faini jumla Sh49,000.

“Lipa mapema kabla faini haijaongeza deni tena- Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini-Tarura,”imeeleza.

 Lakini @ SavageBoe ameandika “mimi pia hii imenikuta sana huwa sielewi muda mwingine inabidi nilipe tu.

Leo Ijumaa Aprili 8, 2022  uongozi wa Tarura makao makuu Dodoma, umetoa taarifa ya kusititisha mchakato huo na kuongeza muda wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mfumo huo.

“Kutokana na kuongeza muda wa utoaji wa elimu kwa wananchi, utozaji wa faini za kuanzia Machi Mosi, unasitishwa kwa muda kuanzia leo Aprili 8 mwaka huu hadi itakapoelezwa tena. Tarura inaendelea kusisitiza wananchi kulipa ushuru wa maegesho kwa wakati.

“Yaani ndani ya siku 14 tangu walipotumia maegesho, kama inavyoelekezwa katika Kanuni za Maegesho, Tangazo la Serikali la namba 799 la Disemba 3, 2021,” imeelezza taarifa hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mfumo wa matumizi ya kieletroniki (TeRMIS) unatoa nafasi ya kupata taarifa za kumbukumbuka za madeni ya ushuru wa maegesho kupitia simu zao za mikononi kupitia Apps za Termis na Gepg.