TASAC waweka mkakati kudhibiti umwagikaji mafuta baharini

Muktasari:

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeandaa mafunzo yatakayohusisha wadau wa mafuta nchini ili kudhibiti umwagikaji wa mafuta baharini unaoathiri maisha ya binadamu na viumbe vya baharini.

Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeandaa mafunzo yatakayohusisha wadau wa mafuta nchini ili kudhibiti umwagikaji wa mafuta baharini unaoathiri maisha ya binadamu na viumbe vya baharini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 16, Meneja wa Viongozi wa Meli, Selestine Mkenda amesema hofu iliyopo kwa sasa ni namna ya kupamabana iwapo kutatokea umwagikaji mkubwa mafuta na kusiwepo na vifaa vya kutosha kudhibiti.

Hata hivyo, Mkenda aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Abdi Mkeyenge, amesema kwa sasa athari sio kubwa.

"Mafuta yaliyosafishwa yakimwagika kwa kiasi kidogo yanaweza yasiwe na athari kubwa sana kwasababu yanayeyuka kwa jua tofauti na mafuta mazito (ghafi), kwani hata yamwagike kwa kiasi kidogo changamoto yake ni kubwa," amesema Mkenda.

Kwa upande wake Mhandisi wa kampuni za mafuta, John Bernad amesema kuundwa kwa timu ya pamoja kwa ajili ya kutafuta suluhisho endapo ikitokea mafuta yakamwagika kwa dharura baharini.

"Mafuta sisi tunayaingiza katika bandari na yana tabia hatarishi zinazoweza zikahatarisha afya ya binadamu na viumbe hai vilivyopo baharani.

“Kwa sababu tunayapokea kwa wingi mkubwa hatari yake ni kubwa zaidi sasa kuwa na shirikisho la pamoja kwa ajili ya kushughulikia inapotokea ajali, hivyo ni muhimu kuwa na vifaa, timu pamoja na mafunzo," amesema John.

Naye Mratibu wa kupambana na uchafuzi wa bahari kwa upande wa Zanzibar, Mhandisi Khalfan Hamad Hassan amesema kuundwa kwa umoja huo kutaleta tija, kwani kwa sasa hali ni mbaya.

"Wito wangu ni wadau kuwa tayari kuanzisha umoja huu haraka iwezekanavyo hata kama ni kesho, ili tuanze kukusanya nguvu na kununua vifaa," amesema.

Clever Mwaikambo kutoka hifadhi za bahari na maeneo tengefu amesema walianza kushughulikia mpango huo wa kudhibiti umwagikaji wa mafuta baharini tangu mwaka 2016.

Alisema marekebisho yalifanyika ndipo wakaja na mpango mpya kwa mwaka huu ambao unaohitaji sekta binafsi zihusike katika suala hilo.

"Tulikwenda kutembelea nchi nyingine na kugundua kitu kinachotakiwa kufanyika sasa kuna umoja wa hiyari na ndio maana leo tuko hapa na kampuni za mafuta kuwaelekeza utaratibu huo.

Amesema utaratibu huu sio mpya, kwani nchi za Angola, Nigeria na Kenya tayari zinao.

"Mafuta yanapomwagika kwenye mazingira ya bahari yanaharibu hata lishe, kwani samaki wanapokula zile chembechembe za mafuta inakuwa ni shida.

“Haiwezekani kurudisha mazingira yaliyoharibika kutoka kwenye uchafuzi wa mafuta na tumeona wenzetu wa Kenya, Nigeria wameshindwa, hivyo inabidi kujikinga kabla ya hatari," amesema Mwaikambo.