TASAC yapewa rungu kuwachongea serikalini wanaowakwamisha
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akizungumza na Menejementi ya Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac), baada ya kukutana leo jijini Dar es Salaam. Picha na Sute Kamwelwe.
Muktasari:
- Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeagizwa kutoa taarifa serikalini kwa wale wote wanaokwamisha katika kutekeleza majukumu yao ili Serikali iweze kushughulikia.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameitaka Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC), kuhakikisha linatenda majukumu yake ili kufikia malengo sambamba na kutoa taarifa serikalini kwa wale wote wanaokwamishia majukumu ya shirika hilo.
Amesema kufanya hivyo kutawezesha Serikali kushughulikia changamoto hiyo katika utendaji kazi ikiwemo kuhudumia bandari zilizopo nchini.
Kihenzile ametoa kauli hiyo leo Septemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na Menejimenti ya shirika hilo likiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Nelson Mlali.
Amesema lengo ni kuongeza ufanisi wa utendaji kwakuwa kwa sasa Shirika hilo linahudumia mizigo tani milioni 24 za mizigo, ambapo inawezekana kupokea na kuhudumia hadi tani milioni 40.
"Kama mnaona kuna changamoto ambazo hamzisababishi ninyi zileteni serikalini tuzifanyie kazi. Kwa sababu haiwezekani unaboresha huduma halafu mtu mfano pale Mikumi na ni mtu wa Serikali anakwamisha malori kwa siku tatu halafu mnamfumbia macho.
Amesema mtu yeyote anayeleta usumbufu hata ambaye sio wa shirika hilo lazima taarifa zitolewe ili wakae naye chini aeleze lengo lake ninini.
"Leo wenzetu Mombasa wanahudumia tani za mizigo milioni 30, Durban 50, halafu sisi 24 na tuna mazingira mazuri na Serikali inazidi kuwekeza ikiwemo kuboresha reli ya Tazara kwa hivyo kwa uwekezaji huu lazima na ufanisi uongezeke," amesema Kihenzile na kuongeza...
"Nimeona mmechangia kwenye mfuko wa Serikali Sh104.5 bilioni kwa kipindi cha miaka minne ambapo mnavituo 16 vinavyohudumia bandari 86. Niwapongeze katika hili na hivyo lazima muangalie mikakati yenu ili kuisaidia Serikali katika kufikia malengo," amebainisha.
Aidha amesema changamoto zote zinazoikabili shirika hilo Serikali itazifanyia kazi ili kuongeza utendaji kazi wa shirika hilo kwa kuongeza mizigo.
Awali akifungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Nelson Mlali amesema shirika liko tayari kufanyia kazi maagizo ya wizara pamoja na kupokea ushauri na maelekezo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuinua uchumi wa nchi.