TBL: Kuleni chakula kabla ya kunywa

Mesiya Mwangoka ambaye ni Mkurugenzi wa masuala ya Kampuni na uendelevu ABInBev, Tanzania na John Blood Mkuu wa masuala ya kisheria na ya Kambuni -ABInBev wakizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya Mdogomdogo

Muktasari:

  • Wakati kampeni za kupunguza matumizi ya pombe yaliyokidthiri zikiendelea kuzinduliwa, wanywaji pombe wameshauriwa kula na kunywa maji mengi kabla ya kunywa ili kupunguza athari za kiafya wanazoweza kupata.

Dar es Salaam. Ili kufikia lengo la kupunguza matumizi ya pombe hatarishi kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imezindua kampeni ya Mdogomdogo inayohamasisha unywaji pombe usiozidi kipimo ambao ni hatari kwa afya ya watumiaji.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umekwenda sambamba na uongezaji wa alama nyingine mbili ambazo zinahamasisha kula na kunywa maji mengi kabla ya kunywa na kunywa kistaarabu.

Alama hizo mbili zilizoongezwa kuungana na tatu zilizokuwapo awali zilizokuwa zikizuia matumizi ya pombe kwa walio na umri wa chini ya miaka 18, kuzuia matumizi ya pombe kwa wajawazito na kutoendesha gari baada ya kunywa.

Hayo yameelezwa katika uzinduzi wa kampeni hiyo inayotarajiwa kudumu kwa miezi 9 hadi Desemba mwaka huu.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo jana Machi 22, Mesiya Mwangoka ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Mahusiano na maendeleo uendelevu wa TBL amesema alama inayohamasisha kula kabla ya kunywa imeongezwa.

Amesema uongezwaji huo umefanyika baada ya utafiti kubaini kuwa kula na kunywa maji mengi kunapunguza uwezo wa mtu kunywa pombe nyingi.

“Unapokula chakula kiwango cha unywaji bia kinashuka, ile bia inaenda taratibu kwa sababu tumbo limejaa tayari na kuna tofauti kubwa ya unywaji imeonekana kati ya yule aliyekula na kushiba na yule anayekunywa bila kula,” amesema Mesiya.

Amesema mtu anapokuwa amekula haimsadii tu kupunguza kiasi cha pombe anachokunywa bali pia kuwa na nguvu na kuzuia mwili wake kudhoofika.

Kampeni ya mdogomdogo pia imelenga kukuza utumiaji bora wa pombe usioathiri desturi za kijamii na tabia ya mtu binafsi na kupunguza matumizi hatari ya pombe.

John Blood ambaye ni Mkuu wa masuala ya kisheria ya kampuni, ABInBev amesema ni muhimu kusaidia watumiaji kuelewa jinsi pombe inapaswa kutumiwa kwa kuzingatia ukomo.

“TBL inahakikisha kuwa masoko yao hayalengi watumiaji wa chini ya umri wa miaka 18, kampuni inalenga kuepuka kukuza utumiaji wa pombe hatarishi au tabia hatarishi zinazotokana na pombe,”