TCC yasambaza madumu ya kuweka uchafu wilayani Temeke

Muktasari:

Ili kutekeleza kampeni  ya Temeke bila uchafu inawezekana kampuni ya sigara Tanzania (TCC) imetoa madumu 241 kwa ajili ya kuhifadhia takataka yatakayosambazwa maeneo mbalimbali wilayani humo.

Dar es Salaam. Ili kutekeleza kampeni  ya Temeke bila uchafu inawezekana kampuni ya sigara Tanzania (TCC) imetoa madumu 241 kwa ajili ya kuhifadhia takataka yatakayosambazwa maeneo mbalimbali wilayani humo.

Utoaji wa madumu hayo umekwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanywa na Mkuu wa wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva.

Akizungumza wakati wa  kuyakabidhi  leo Ijumaa Desemba 13, 2019 meneja ubora na mjumbe wa kamati ya mipango endelevu, Neema Ngoitiama amesema madumu hayo uhifadhi gundi kwa ajili ya kutengenezea bidhaa zao na pindi zinapomalizika husafishwa kitaalamu na kugawiwa kwa wafanyakazi.

“Wakati wageni walipokuja katika mkutano wa SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika), halmashauri ilitoa taarifa kila ofisi iliyo karibu na barabara ya Nyerere kuwa na vifaa vya kuhifadhia taka,  tuliweka mapipa 10 yaliyoonyesha matokeo chanya tukaona kumbe tunaweza kulifanyia maboresho wazo letu,” amesema.

 

Amesema baada ya wageni kuondoka waliamua kufanya usambazaji wa mapipa hayo kwa halmashauri ya Temeke katika awamu ya kwanza na baadaye wilaya nyingine.

“Tutaendelea kutoa mapipa 50 kila mwezi kwa halmashauri hii hadi pale watakaposema yametosha basi tutaelekeza nguvu zetu katika halmashauri nyingine ndani ya jiji na hatimaye mikoani,” amesema Neema

Lyaniva amezitaka halmashauri hizo kuhakikisha zinatunza mapipa hayo na yatumike kama yalivyokusudiwa kuendeleza kampeni hiyo.

“Nimeizindua kampeni hii ambayo ni endelevu, tunataka wilaya yetu iwe safi na madumu haya yapelekwe katika mitaa yote 142 ziliyopo katika wilaya yangu hasa sehemu zinazozalisha takataka kwa wingi,” amesema Lyaniva.